WANANCHI WAASWA KULINDA HIFADHI HAI YA RUMAKI ILI IBAKI KWENYE UBORA WAKE
Wananchi wa Mkoa wa Pwani na maeneo yote nchini wameaswa kulinda na kuyatunza maeneo maalumu yaliyotengwa na Serikali kwa kuacha uvamizi kwenye maeneo hayo muhimu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Khamis Hamza Khamis alipokuwa akizindua Hifadhi hai mpya ya RUMAKI Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Naibu Waziri amewapongeza wadau wa Mazingira kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha mazingira yanalindwa pia amewaasa wananchi kuacha tabia ya uvamizi, uvuvi haramu na ukataji wa miti kwenye Hifadhi hai ili kutunza Mazingira.
“Kumekuwa na tabia ya wananchi kwenda kuvamia maeneo ya Hifadhi hai kwa kukata miti, kufanya uvuvi haramu na shughuli nyingine za kibinadamu hivyo niwaombe twendeni tukayalinde maeneo hayo tengefu ili yakawe salama. Hata hivyo hili litafanikiwa iwapo tu wanajamii na wadau wote tutaungana na kuweka juhudi zetu katika kuhamasisha na kuchukua hatua kuhakikisha maliasili zetu zinaendelea kulindwa na kuhifadhiwa” amesema Mhe. Naibu Waziri Khamis Hamza.
Kadhalika Mhe. Khamis Hamza amelitaka Baraza na wadau wengine wa Mazingira kutoa elimu na kuwashirikisha wananchi kwenye miradi ya Uhifadhi wa Mazingira.
“NEMC na Taasisi zote zinazohusika kuratibu miradi kama hii muwe na utaratibu maalumu wa kuwaelimisha wananchi faida za maeneo tengefu na hasara zitakazotokea endapo watavamia maeneo hayo pia ninaomba ushirikishwaji wa wananchi kwenye miradi mingine yote inayolenga utunzaji na uhifadhi wa Mazingira “ amesema Mhe. Khamis Hamza.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan Jangu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC amesema utayari wa wananchi umefanikisha kutambulika kwa Hifadhi hai hivyo zinatakiwa kulindwa huku shughuli za kibinadamu zinaendelea bila kuathiri Hifadhi hizo na Mazingira kiujumla.
Programu ya Binadamu na Hifadhi Hai ni jukwaa lililo chini ya UNESCO, ambalo linashughulika na kuanzisha, kukuza na kuweka uhusiano sawia kati ya binadamu na uhifadhi. Na kwa Tanzania Programu hii inaratibiwa na kamati ya Kitaifa chini ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15