UZINDUZI RASMI WA MRADI WA UHIMILI WA MABADILIKO YA TABIANCHI - PWANI ZA ZANZIBAR


Warsha ya mafunzo ya Mradi wa Kuimarisha uhimili wa mabadiliko ya Tabianchi kwa Jamii ya Pwani za Zanzibar wazinduliwa rasmi. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa ASSP Maruhubi Mjini Zanzibar.

Warshahiyo imefunguliwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Dkt. Omar D. Shajak na kuhudhuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Wengine walioshiriki katika warsha hiyo ni watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Watumishi wa NEMC na Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali.

Dkt. Omar Shajak amesema kuwa mabadiliko ya Tabianchi ni janga la Kidunia hivyo, hatuna budi kukabiliana nayo. Amesema juhudi mbalimbalizimechukuliwa ilikupambana na mabadiliko hayo ikiwemo kuwepo kwa Sera, Sheria na mifumo ya Kitaasisi ya usimamizi wa mabadiliko ya Tabianchi.

Katika uzinduzi huo Dkt.Shajak ameishukuru na kuipongeza NEMC kwa juhudi kubwa walizochukua katika kupatikana kwa fedha za mradi kupitia Mfuko wa Uhimili wa mabadiliko ya Tabianchi(Adaptation Fund) ambao leo hii unazinduliwa rasmi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake, pia amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP kwani wao ndio chimbuko la kupatikana kwa andiko la mradi huu.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Dkt. Samuel Gwamaka ameipongeza Zanzibar kuwa wa kwanza kupata fedha kwa ajili ya mradi wa kuimarisha uhimili wa mabadiliko ya Tabianchi kwa jamii ya Pwani za Zanzibar kupitia Mfuko wa adaptation fund.

“Kuwa wa kwanza ni jambo linaloleta wajibu wa kuonesha mfano katika utekelezaji ili wanufaika watakaofuata waweze kujifunza. Siyo hivyo tu bali utekelezaji wenye ufanisi utavutia hata wafadhili wengine kuweka fedha zaidi kwenye mfuko kwa ajili ya kuendeleza kazi zilizoanzishwa na mradi huu sambamba na kulipatia Taifa letu sifa nzuri katika Jumuiya ya Kimataifa” Dkt. Gwamaka"

Dkt. Gwamaka amemaliza kwa kusema kuwa NEMC wataendelea kutoa ushirikiano na Msaada wowote utakaohitajika kusudi mradi huu uweze kutekelezeka na kukamilika kwa wakati huku mafanikio yake yakionekana na kudumu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.