RAI YATOLEWA KWA WAMILIKI WA BAA NA KUMBI ZA BURUDANI KUZINGATIA SHERIA KATIKA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZAO


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamzi wa Mazingira NEMC limewataka wamiliki wa kumbi za starehe na baa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake wakati wa uendeshaji wa shughuli za burudani.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt Samuel Gwamaka alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa NEMC uliopo Jijini Dar es salaam.

Amesema uendeshaji wa shughuli za burudani usiozingatia Sheria ya Usimamizi wa mazingira umepelekea kukithiri kwa sauti zilizozidi viwango hali inayoleta kero kwa wananchi wanaozunguka maeneo yenye vizalisha sauti hizo

“Ni wazi kabisa wamiliki wa baa, kumbi za burudani wamejisahau, tulipotoa elimu ya udhibiti wa sauti zilizozidi viwango, na kufungia baadhi ya mabaa, na nyingine kutozwa faini, hali ilipungua, lakini sasa naona upo ulazima wa kuwakumbusha tena kwani hali imerudi kama mwanzo” Amesema Gwamaka

Ameeleza kuwa kama Baraza wajibu ilionao ni kuwakumbusha wamiliki wote wa mabaa na kumbi za burudani kuzingatia Sheria ili kuepukana na athari au changamoto zinazosababishwa na uzalishwaji mkubwa wa sauti zilizozidi viwango katika jamii na kuleta athari.

“Kama baraza tunawakumbusha kwamba Sheria bado ipo na inafanya kazi, tunaendelea kuwaelimisha kwamba kelele bado ni kero na zinawagusa hata wasio husika” Amefafanua Dkt. Gwamaka

Amezitaja athari zinazosababishwa na sauti zilizozidi viwango kuwa ni uziwi, wagonjwa kushindwa kupumzika, wanafunzi kushindwa kujisomea, watu kuhama makazi, mimba kuharibika, kuwakosesha wazee muda wa kupumzika pamoja na magonjwa ya Moyo.

Katika hatua nyingine Dkt Gwamaka alipokuwa akifafanua hoja ya matumizi ya nishati kama chanzo cha uharibifu wa mazingira, amesema azma ya Baraza kufikia 2025 kuwe na ongezeko kubwa la matumizi ya gesi asili ili kupunguza uharibifu wa Mazingira.