NI MUHIMU KULINDA NA KUHIFADHI MAZINGIRA ZIWA VICTORIA - DKT. JAFO


Wadau mbalimbali wametakiwakuendeleza jitihada za Serikali za kulinda ziwa Victoria dhidi ya vitendo vya uchafuzi wa mazingira kutokana na umuhimu wake kwa shughuli za maendeleo kwa watu wa Afrika.

Wito huo umetolewajijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo, wakati akizindua Mpango Mkakati wa kusimamia Mazingirakatika Ziwa Victoria.

Mpango huo unaratibiwa na Kituo cha Sayansi ya Mazingira Center for Science Environment (CSE) cha nchini India ambacho kimekuwa kikitafiti chanzo cha uchafuzi wa ziwa hilo na kutafuta majibu yake.

Waziri Jafo alisema kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwenye ulinzi na usafi wa ziwa Victoria ambalo limekuwa tegemeo kubwa kwa mamilioni ya watu wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Alisema ziwa hilo limekuwa chanzo kikubwa cha maji ya Mto Nile ambao unategemewa na zaidi ya watu milioni 40 kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kilimo na uvuvi.

“Hili ziwa ni kubwa sana na linategemewa zaidi duniani kwasababu maji yake ndiyo uchumi wa wenzetu kwa hiyo ninapoona wadau kama nyinyi mnajitokeza kulilinda inanipa moyo sana, wenzetu Misri wanategemea sana mto Nile ambao unapata maji kupitia ziwa Victoria, ” alisema

Alisema amefarijika kuona wageni mbalimbali wametembelea ziwa hilo na kukuta halijachafuliwa kama ambavyo imekuwa ikitokea hasa wakati wa kipindi cha mvua hivyo alitaka hali hiyo ya usafi iwe endelevu.

“Ukitembelea ziwa Victoria msimu ambao hauna mvua unaweza kudhani kwamba hali ndivyo ilivyo siku zote lakini mvua zikianza ndipo utaona hali halisi ya mazingira yake. Wageni wetu wameenda wamekuta safi sasa hali hii iendelee hata msimu wamvua,” alisema Waziri Jafo.

Aidha, Waziri Jafo aliipongeza ushirikiano mwema uliopo baina ya serikali ya Tanzania na India ambayo alisema kwa sasa inafadhili miradi 28 ya maji yenye thamani ya zaidi ya trilioni moja kwenye mikoa mbalimbali nchini na tayari imeshaanza kujengwa.

“Serikali ya India inatusaidia sana kwenye mambo mengi sasa ninapoona na nyinyi mmekuja kutusaidia kulinda ziwa Victoria dhidi ya uchafuzi wa mazingira yake inazidi kunipa amani ya moyo kwamba nyinyi ni ndugu zetu na mnapenda maendeleo yetu,” alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CSE, Dk. Sunita Narain, alipongeza jitihada zinazofanywa na serikali kulinda na kuhifadhi mazingira na kwa namna ambavyo kituo hicho kimepata mapokezi mazuri.

“Tunaishukuru serikali ya Tanzania kwa kutupokea vizuri tangu tulipofika nchini mwezi uliopita, tumetembelea ziwa Victoria kujionea hali ilivyo na tumeridhika kwa namna mikakati inavyowekwa kulilinda dhidi ya uchafuzi,” alisema Dk. Suniti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, alisema Baraza limekuwa na ushirikiano wa karibu na Kituo cha Sayansi na Mazingirakilichopo nchini India.

Alisema wanashirikiana katika kuandaa shughuli mbalimbali za kimazingira ikiwa ni pamoja na uandaaji wa Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Mazingira kwa Ziwa Victoria na kwamba uandaaji wa mpango huo umezingatia miongozo mbalimbali ya nchi.

“Uanzishaji wa mkakati huu ni jitihada za Baraza katika utekelezaji wa Mkakati Kabambe wa Mazingira wa Taifa wa Mwaka 2022/32 uliozinduliwa rasmi mwezi Juni 2022 na pia Ajenda ya Taifa ya Tafiti za Mazingira (2017/22),” alisema Dk. Gwamaka.