​NEMC YAWATAKA WAMILIKI WA MABASI KUZINGATIA UTUNZAJI WA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wamiliki wa mabasi kuzingatia Utunzaji na Uhifadhi wa mazingira kwa kuweka vyoo na vitenganishi taka kwenye mabasi yao wanapokuwa safarini.

Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Mafwenga Gwamaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na abiria kwenye mabasi pamoja na namna sahihi ya kudhibiti uchafuzi huo katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa NEMC Dar es Salaam.

Amesema abiria wa mabasi wamekuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira kwa kutupa taka madirishani na kuchimba dawa maporini wakati wa safari ndefu hali inayopelekea kuhatarisha maisha yao pamoja na kuchafua mazingira hasa vyanzo vya maji.

"Kumekuwa na tabia ya abiria kutupa mabaki ya vyakula madirishani popote pale, au kwenda haja kubwa na ndogo wakati wa safari ndefu, barabarani, huko kuna hifadhi za misitu, kuna mbuga za wanyama, kuna hifadhi za barabara, zote hizi zinatakiwa kulindwa, kwa maana hiyo uuchafuzi wa aina hiyo sio mzuri kwanza ni kuchafua mazingira, lakini pia ni kuathiri afya, na kubwa zaidi ni kudhalilisha wanawake" amesema Dkt. Gwamaka.

Ameongeza kuwa mabasi yote ya abiria wa safari ndefu yanapaswa kuzingatia Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira kwa kuweka vitenganishi vya taka kwenye mabasi hali itakayosaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira.

Amesisitiza kuwa uchafuzi wa aina hii una athari kubwa katika mazingira kwani huibua magonjwa ya mlipuko, husababisha kuchafuliwa na kuziba kwa vyanzo vya maji hupelekea mikondo ya maji kuziba, husababisha mchafuko wa hali ya hewa pamoja na kuharibu ikolojia ya wanyama na mimea.

Amezitaka Halmashauri kote nchini kwa kushirikiana na TABOA pamoja na LATRA kuhakikisha elimu ya utunzaji wa mazingira inatolewa na kujenga vyoo maeneo husika ili kuepukana na adha hiyo ya uchafuzi wa Mazingira.

Katika hatua nyingine amewataka wenye viwanda kuhakikisha wanazingatia mpango wa kutunza mazingira kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuhifadhi taka za viwandani na majumbani ili kutunza Mazingira.

Pamoja na hayo ameitaka jamii ya watanzania kuwa na tabia ya kutenganisha taka za plastiki, kielekroniki, chuma, karatatasi na mabaki ya vyakula kuanzia majumbani ili kupunguza mzigo kwa Halmashauri wa ukusanyaji wa taka kwani taka ni fursa zinaporejerezwa na kutoa ajira pamoja na malighafi nyingine za viwandani