NEMC YATOA WITO KWA WAANDISHI WA HABARI KUJIFUNZA MASUALA YA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa wito kwa waandishi wa habari kuwekeza nguvu zao kujifunza masuala ya mazingira ili waweze kuwa na uwasilishaji mzuri wa habari za Mazingira kwa wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika Jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC Bi. Irene John ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa programu maalumu ya kuwaleta pamoja waandishi wa habari ili kuongeza uelewa wa masuala ya Mazingira, programu inayolenga kuongeza umahiri na uwasilishwaji wa habari za Mazingira kwa jamii. Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Mikoko Launge Jijini Dar es salaam.

Bi. Irene amesema ni wajibu wa kila Mwandishi kuweka nguvu zaidi katika kujifunza na kufanya tafiti za mazingira kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za uhifadhi na utunzaji wa Mazingira. Wanahabari ni lazima kutumia lugha nyepesi itakayoeleweka na jamii hususani masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi na pia kuyaishi yale yanayowaelimishia wengine kuhusu Utunzaji wa Mazingira kwa ajili ya kuleta matokeo chanya.

“Niwaombe waandishi na wahariri wa habari wote tujifunze zaidi kuelewa masuala ya mazingira kama elimu ya utenganishaji wa taka, uchumi wa buluu na mabadiliko ya Tabianchi. Kama mimi na nyie tusipoelewa ni ngumu kuelimisha jamii, niwaombe sana elimu ya utunzaji wa Mazingira ianzie kwetu sisi wahariri na waandishi wote tuliopo hapa tuyaishi yale mambo tunayoelimisha jamii “ amesema Bi. Irene John

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya TMF Bw. Dastan Kamanzi amewataka waandishi hao kuandika habari za Mazingira zinazolenga kuongeza uelewa, ujuzi na kuleta mabadiliko katika jamii. Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa HUDEFO Bi.Sarah Pima ameishukuru sana NEMC kwa kushirikiana nao katika uzinduzi wa programu yao maalamu inayolenga kuwajengea uwezo waandishi hasa wahariri wa habari za Mazingira ili waweze kutoa taarifa sahihi za Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira kwa ajili ya manufaa ya Taifa zima.

Katika hatua nyingine za uchangiaji wa masuala ya uhifadhi na utunzaji wa Mazingira naye Profesa Hamudi Majamba toka chuo kikuu cha Dar es Salaa aliongezea kuwa Mazingira ni jambo mtambuka linagusa jamii moja kwa moja hivyo tusipoyatunza yatatuadhibu. Amewasisitiza waandishi kutumia lugha nyepesi mfano badala ya kusema ozone layer kwa wananchi wa kawaida tuite blanketi inayosaidia kuzuia miali ya jua kushuka moja kwa moja duniani ambapo hilo blanketi likizidiwa na joto kali ndo tunapata mabadiliko ya tabianchi nchi ikiwa ni pamoja na joto kali, vimbunga na mafuriko.

Programu tajwa imeratibiwa na Taasisi ya HUDEFO kwa kushirikiana na TMF.