NEMC YATOA VIFAA NA KUSHIRIKI ZOEZI LA USAFI -KISUTU


NEMC YATOA VIFAA NA KUSHIRIKI ZOEZI LA USAFI -KISUTU

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira kwa kushiriki katika zoezi la usafi kwenye baadhi ya maeneo ya mtaa wa Kisutu. Zoezi hilo limefanyika leo tarehe 07 Mei 2022 pamoja na kutoa vifaa vya kufanyia usafi kama fagio,vikinga mikono na barakoa kwa Kampuni ya Orbit Media inayoshirikiana na serikali ya mtaa wa Kisutu jijini Dar es salaam ili kuwezesha wananchi kutunza mazingira katika maeneno mbalimbali ya jiji.

Akikabidhi vifaa hivyo vya usafi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bi. Irene John amesema " Tumefurahi leo kuungana na wenzetu mahali hapa kufanya usafi kwa sababu ni jukumu letu kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi na salama. Maana jiji letu likiwa safi hatutaona magonjwa kama kipindupindu, lakini pia miili yetu itakua na afya njema na kuongeza nguvu kazi ya Taifa katika kukuza uchumi. Hivyo NEMC inatoa wito kwa taasisi nyingine wajitoe katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa Miji na Majiji yanakuwa safi na salama."

Naye Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kisutu Bi. Mariam Bawaziri ameishukuru NEMC kwa kutoa vifaa pamoja na kushiriki zoezi la kufanya usafi katika baadhi ya maeneo ya mtaa wa Kisutu ikiwa ni moja ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa kwa kuhakikisha kuwa jiji linakuwa safi.

Aidha Mkurugenzi wa kampuni ya Orbit Media Bw. Moses Mwakibolwa ametoa shukrani kwa NEMC baada ya kupokea vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya zoezi la usafi wa jiji. Pia ameishukuru Serikali ya mtaa wa Kisutu pamoja na wadau waliojitokeza kufanya usafi na kutoa pongezi kwa Serikali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kuhimizia usafi kwa kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara.

Kwa upande wake mmoja wa wanachi wa mtaa wa Kisutu Bw. Leonce Safari ameishukuru NEMC kwa kutoa vifaa na kushiriki zoezi la usafi katika mtaa wa Kisutu na kuishukuru Serikali kwa ajili ya kubuni zoezi hilo na kuahidi kuvitumia vifaa hivyo katika kutekeleza kampeni ya kuweka jiji safi kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji.