​NEMC YATOA HUDUMA NANENANE, WANANCHI WAKARIBISHWA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeanza kutoa huduma katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo maarufu kama Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Hayo yamebainishwa Julai 31, 2023 na Kaimu Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini - NEMC Bw. Josiah Murunya alipokuwa akiwakaribisha wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa mazingira kutembelea banda la NEMC katika maonesho hayo.

Bw. Josiah Murunya amesema katika maonesho hayo NEMC inatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusajili wataalmu elekezi wa Mazingira, kusajili miradi kwa ajili ya cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kutoa elimu ya mazingira na kupokea malalamiko na ushauri kutoka kwa wadau.

“Tunatoa huduma za usajili wa wataalamu elekezi wa mazingira, usajili wa miradi kwa njia ya mtandao, kutoa elimu kuhusiana na uhifadhi na utunzaji wa mazingira na tunapokea malalamiko na maoni kutoka kwa wananchi na kuyafanyia kazi moja kwa moja hapa bandani” Amesema Bw. Josiah.

Naye Afisa Elimu ya Jamii Mwandamizi wa NEMC Bi. Suzan Chawe amewakumbusha wawekezaji wa miradi juu ya takwa la Sheria ya Mazingira linaloelekeza kusajili miradi na kufanya Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM).

“Baraza limerahisisha mchakato wa TAM kwa kuanzisha usajili wa miradi kwa mfumo wa kielektroniki (online registration) na kusogeza huduma katika ofisi zetu za Kanda zinazopatikana Tanzania nzima”. Amesema Suzan Chawe.

Aidha, Bi. Suzan amewakaribisha wenye sifa za kuwa washauri elekezi wa Mazingira kujisajili na kupata cheti cha utendaji kwa ajili ya kufanya TAM na ukaguzi wa mazingira.

Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linawaalika wananchi na wadau wote wa mazingira kutembelea banda lao lililopo Viwanja vya John Mwakangale kwa ajili ya kupata elimu juu Utunzaji na Uhifadhi wa mazingira.