NEMC YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MAZINGIRA KIMKOA
NEMC YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MAZINGIRA KIMKOA
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limeshiriki maadhimisho ya Mazingira Duniani, yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya Mwinjuma vilivyopo Kata ya Makumbusho Manispaa ya Kinondoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali.
Akiongea katika Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo Pinga uchafuzi wa Mazingira utokanao na mifuko ya plastiki mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila amesema, Mkoa wake unaungana na wadau wa Mazingira pamoja na wananchi kote dunani kuiadhimisha sikuu hii muhimu ya Mazingira kwa kaulimbiu thabiti yenye kuweka mkazo matumizi sahihi ya vifungashio na sio mifuko ya plastiki kama vibebeo ili kutunza mazingira.
Ameongeza kuwa kauli mbiu hii inatoa chagizo kwa kila mwananchi katika Mkoa wake kuelewa maana halisi ya kuhifadhi mazingira na kuachana na matumizi ya mfuko ya plastiki iliyokatazwa kwa mujibu wa Kanuni za mwaka 2019 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali namba 304.
‘Mkoa wa Dar es salaam ni Jiji la biashara, hivyo uchafuzi wa mazingira kwa mifuko ya plastiki umekuwa dhahiri kabisa, na hii inatokana na uwepo wa viwanda bubu vingi, lakini pia Mkoa wangu umekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza katazo hili la mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na NEMC pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa hivyo jitihada ni kubwa lakini hazitoshi bila nyie wananchi wenzangu kutuunga mkono’ amesema Albert Chalamila.
Naye Bi Glory Kombe akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu NEMC amesema wajibu ilionao taasisi yake ni kuishauri Serikali katika masuala ya Mazingira, lakini pia ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya waka 2004 na Kanuni zake na kwamba imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha agizo la Serikali la kutokomeza mifuko ya plastiki linatekelezwa kwa weledi na kwa wakati.
Amesema NEMC inaendelea kutoa elimu ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira, lakini pia inaendelea kufanya kaguzi mbalimbali kwenye viwanda na masoko, huku ikihakikisha viwanda bubu vinadhibitiwa kwa mujibu wa Sheria.
Maadhimisho hayo yaliyosheheni burudani mbalimbali yamehudhuriwa pia na viongozi wa vyama na Serikali, Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaa, TFS, pamoja na wadau wa Mazingira.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15