NEMC YARIDHISHWA NA MRADI WA RELI YA KISASA (SGR)
NEMC YARIDHISHWA NA MRADI WA RELI YA KISASA (SGR)
Bodi ya wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), imefanya ziara katika mradi wa reli ya kisasa(SGR) na kushauri masuala mbalimbali ya mazingira.
Hatua hiyo ya NEMC ni utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Bunge, Uwekezaji, Viwanda na Mazingira ambapo waliagiza miradi ya kimkakati inapojengwa Baraza hilo lifuatilie kwa karibu badala ya kusubiri athari zitokee ndio hatua zichukuliwe.
Akizungumza leo Juni 14,2022, katika ziara hiyo ya ukaguzi kutoka Dar es salaam hadi Ruvu, Mwenyekiti Bodi hiyo, Prof.Esnath Chaggu, amesema wamefika kukagua uzingatiaji wa masuala ya mazingira katika mradi huo mkubwa wa muhimu kwa taifa.
“Usafirishaji kwenye nchi yetu ni suala la muhimu sana ndio maana mradi huu mkubwa umeanzishwa, kwa taarifa ambazo tumezipata uzingatiaji wa masuala ya mazingira unafanyika vizuri sana na wanafuatilia kwa karibu,”amesema.
Amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeamua kuanzisha kitengo maalum kinachohusika na mazingira ambapo wanahakikisha kwamba wameajiri wataalamu wa mazingira.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk.Samuel Gwamaka, amesema ziara ni utekelezaji wa kamati hiyo ili kutosubiri athari zitokee ndio baraza lichukue hatua.
“Hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza miradi hii mikubwa ya maendeleo sisi Baraza NEMC tuwe karibu nayo ili kushauri pale mambo hayaendi vizuri ya kimazingira,”amesema.
Amebainisha kuwa katika ziara hiyo wamezungumza na Menejimenti ya TRC ambapo miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa ni kero ambayo wananchi wamekuwa wakiipata wakati wa ujenzi ikiwamo eneo la Kipawa kuwa na mafuriko.
“Tumeshauriana jinsi ya kuchukua hatua ili kusitokee tena tatizo, kuna maeneo mbalimbali kwenye hii SGR walikuwa wamezoea kuyavuka, sehemu kubwa sasa hawataweza kuvuka kutokana na senyenge kubwa ambayo imewekwa kwa usalama wao, maeneo hayo tumeshauri,”amesema.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15