NEMC YAONYA UCHAFUZI WA MAZINGIRA ILI KUDHIBITI MAFURIKO


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wananchi kudhibiti utupaji wa taka ngumu katika njia na mikondo ya maji ili kuepuka mafuriko na mlipuko wa magonjwa katika kipindi cha mvua.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari leo 2 Februari, 2025 katika Ofisi za NEMC jijini Dar es salaam.

"Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa tunaweka Mazingira safi na salama ili kuepusha mafuriko na mlipuko wa magonjwa ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada zetu katika ujenzi wa Taifa. Tunatoa wito Kwa Mamlaka za Serikali za mitaa hususani jijini Dar es Salaam kuchukua hatua stahiki kupambana na watu wanaotupa taka ngumu katika mifumo ya maji pamoja na kuimarisha njia na mikondo ya maji ili iwe safi wakati wote" amesema Dkt. Semesi.

NEMC imetoa wito huo kufuatia taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) iliyotolewa Januari 23, 2025 ikitahadharisha uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Semesi amezitaka mamlaka za Serikali za Mitaa kufuatilia kwa karibu maeneo ya uchimbaji wa madini na vifusi ili kuhakikisha usalama wa jamii husika na kuendelea kufuatilia kwa ukaribu taarifa za hali ya hewa (TMA) ili kuchukua tahadhari ya maeneo yenye viashiria hatarishi.

Sambamba na hilo, Dkt. Semesi ameeleza kuwa mvua hizo zimekuwa zikiathiri makazi ya wananchi, kusababisha uharibifu wa mashamba, upotevu wa mali, na hata vifo. Sekta za kilimo, mifugo, na maji zimekuwa zikiathirika kwa kiasi kikubwa, hali inayoweza kuhatarisha upatikanaji wa chakula na ubora wa maji. Vilevile miundombinu muhimu kama barabara, umeme, na mawasiliano pia imekuwa ikiharibika, hali inayoleta changamoto kubwa kwa wananchi huku uchafuzi wa vyanzo vya maji ukisababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa za matumbo, jambo linalohitaji tahadhari za haraka.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma NEMC, Bi. Irene John ameitaka jamii kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kudhibiti utupaji taka holela na utiririshaji wa maji taka ili kuepuka kuziba kwa mitaro pamoja na magonjwa ya milipuko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Semesi amewakumbusha wananchi kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, Kifungu Namb. 57 na kuepuka ujenzi kwenye maeneo hatarishi ikiwa ni pamoja na maeneo ya kando ya mito, mabonde, fukwe za bahari na maeneo ya ardhi oevu.