NEMC YAIKUMBUSHA JAMII JUU YA ULINZI WA TABAKA LA OZONI
Ikiwa leo ni maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuhifadhi tabaka la Ozoni, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutoa elimu kwa umma na kuwataka wananchi kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kununua bidhaa rafiki wa Ozoni (Ozone friendly) ili kulinda tabaka hilo dhidi ya uharibifu.
Ozoni hili ni tabaka la hewa ambalo liko katika anga la juu la pili lifahamikalo kitaalamu kama stratosphere ambalo linaweka aina ya tabaka ama tambara angani ambalo linazuia mionzi mikali ya jua inayoweza kuleta athari katika afya za binadamu na viumbe hai kuja moja kwa moja duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo hii Afisa wa Mazingira Mwandamizi kutoka NEMC Fredrick Mulinda, amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha bidhaa wanazonunua zinakuwa na nembo rafiki kwa Ozoni (Ozone Friendly) ama nembo ya CFC Free ikiwa na maana hazina gesi zinazoharibu tabaka la Ozoni.
Ameeleza kuwa uharibifu wa tabaka la Ozoni unapelekea madhara mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani pamoja na kuleta mabadiliko ya tabia ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa binadamu na viumbe hai.
Mulinda amesema kuwa ipo programu ya kitaifa ya kutekeleza majukumu kwa ajili ya kuchangia jitihada za kimataifa za kulinda tabaka la Ozoni ikiwemo kutoaelimu katika taasisi pamoja na wanajamii wa ngazi mbalimbali.
“Taasisi kama TBS, TRA pamoja na watu kutoka NEMC wamepata mafunzo juu ya namna ya kulinda tabaka la Ozoni, na zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali kufikisha elimu hii kwa jamii. Sisi NEMC tunafikisha kupitia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijami" amesema Mulinda
Ameeleza pia mafunzo mengine yametolewa katika vyuo vya mafunzo ya ufundi (VETA) hivyo kuwapa fursa mafundi kujifunza namna bora ya kuhudumia vifaa mbalimbali vyenye kutoa gesi ambazo zinaweza kuharibu tabaka la Ozoni.
“Serikali iliunda kanuni ya kuthibiti hizi kemikali pamoja na gesi zinazoharibu tabaka la Ozoni mwaka 2007 ambayo ndio inayotoa mwongozo mkuu wa namna ya kudhibiti bidhaa hizo. Lakini pia tayari upo udhibiti katika uingizwaji wa vifaa vyenye gesi hatari kwa Ozoni ambapo pia vifaa vya utambuzi vimewekwa katika vituo vya forodha ili kutambua bidhaa hizo” ameeleza Mulinda
Kuhusu ushiriki wa NEMC Bw. Mulinda ameongeza kuwa Baraza limeshirikiana na vyuo mbalimbali katika kukuza mitaala yao pamoja na kuingiza elimu ya uhifadhi wa tabaka la Ozoni katika mitaala yao na kuanzishwa taratibu za kuweka mashine katika maeneo ya kalakana na vyuo vya ufundi ili kuwawezesha mafundi mchundo kurejeleza gesi hatari zisiweze kuleta madhara endapo zitakuwa zimetoka.
Hata hivyo, maadhimisho ya mwaka huu yanakuwa ni ya 35 yakiwa na lengo la kuikumbusha Dunia juu ya umuhimu na namna ya kulinda tabaka la Ozoni kwa manufaa ya afya za binadamu pamoja na Mazingira
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15