NEMC YAANDAA MKUTANO WA KAMATI YA TAIFA YA BINADAMU NA HIFADHI HAI MJINI MOROGORO.


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeandaa Mkutano wa kupitia na kuidhinisha uteuzi wa eneo la Rufiji, Mafia, Kibiti na Kilwa(RUMAKI) kuingia katika mtandao wa dunia wa binadamu na Hifadhi hai.

Mkutano huo umefunguliwa na Dkt Menan Jangu aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC na umefanyika mjini Morogoro na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Binadamu na Hifadhi hai kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali.

Aidha akiongea katika Mkutano huo Dkt. Jangu amesema dhumuni kubwa la mkutano huo ni kupitia kwa pamoja na kuridhia mapendekezo ya uteuzi wa eneo la RUMAKI kuingia katika mtandao wa dunia wa binadamu na hifadhi hai kwani kufanya hivyo ni muhimu kwa ustawi wa mazingira.

“Lengo la Mkutano huu ni kupitia mapendekezo na kujiridhisha kwa ajili ya maandalizi ya kuridhia RUMAKI kuingia katika mtandao wa dunia wa Binadamu na hifadhi hai”

Naye Meneja wa Tafiti za Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bi Rose Salema amesema kuwa Hifadhi hai za Taifa ni muhimu sana kwani zinamshirikisha binadamu katika maeneo yake na pia Binadamu atafaidika kwa hizo Hifadhi hai. “Hifadhi hai za Taifa ni muhimu sana na kwa mfano hili la RUMAKI wananchi wa maeneo hayo tutawatafutia miradi na kazi mbadala ili waweze kuondoa uharibifu katika mazao ya bahari”

Kamati ya Taifa ya Binadamu na Hifadhi hai Nchini inaundwa na wajumbe kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali kama vile Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakal wa huduma za misitu (TFS),Chuo Kikuu cha Das es Salaam, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Tafiti za Misitu (TAFORI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI)na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro (NCAA)