NEMC YAWAONYA WAUZAJI CHUMA CHAKAVU KUHUSIANA NA ATHARI KIAFYA


Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Magharibi imebaini wafanyabiashara wa chuma chakavu hawahifadhi vizuri hali inayohatarisha afya za binadamu na kuathiri mazingira.

Kutokana na hali hiyo, imeanza kufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao na wachimbaji madini ili kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mazingira na Kanuni ya usimamizi wa mazingira ya taka hatarishi na taka za kielekroniki za mwaka 2021.

Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha utoaji elimu hiyo kilichofanyika wilaya ya Igunga, Meneja wa Kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi, Edgar Mgila, alisema wafanyabiashara wa chuma chakavu wanahifadhi kwenye maeneo ambayo si salama hayajasakafiwa wala kuezekwa.

“Kwa mfano eneo halina sakafu na wala halijafunikwa juu ni rahisi wakati wa mvua kutiririsha sumu ya chuma inayoweza kusababisha madhara kwenye jamii,”alisema.

Pia, aliwataka kutumia vifaa kinga kwenye ukusanyaji wa taka hizo ili kuepuka kupata magonjwa yanayotokana na sumu hiyo.

Kadhalika, alisema kwenye ukaguzi migodini wamebaini watu wanaochimba na kuchenjua dhahabu kwa kutumia kemikali hawavai vifaa kinga kuzuia kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani.

“Jukumu letu ni kufanya kaguzi na kutoa elimu kwa wadau na kutoa maelekezo tunapofanya kaguzi, kwa kipindi cha mwezi Mei tumefanya ukaguzi Wilaya ya Igunga na Nzega na kutoa elimu ya usimamizi wa mazingira,”alisema.

Alifafanua kuwa kwenye utoaji elimu huo wadau wameelezwa umuhimu wa kutumia vifaa kinga na kutumia vizuri kemikali ili zisisababishe madhara kwa binadamu na mazingira.

Alisisitiza kuwa zoezi hilo linaendelea kwenye maeneo mengine ya kanda hiyo ili wafanyabishara wa vyuma chakavu na wachimbaji ili shughuli za kibinadamu zisiathiri mazingira.

Naye, Diwani wa Kata ya Nguvumoja, Alferd Nkuba, alipongeza NEMC kwa kutoa elimu hiyo kwa wachimbaji kuhusu sheria ya mazingira na kanuni zake ili wazingatie usalama wa afya zao na uhifadhi wa mazingira.

Nao, viongozi wa wafanyabiashara ya chuma chakavu, Boaz Dhahabu na Idaso Mayanda walipendekeza vibali vya chuma chakavu vitolewe kwa wafanyabishara kulingana na mitaji yao ili kukidhi matakwa ya kanuni.

“Pia suala la elimu juu ya uhifadhi na usafarishaji wa taka hatarishi itolewe mara kwa mara ili kuwajengea wafanyabiashra uelewa,”alisema Dhahabu.

Mwisho