MRADI WA BOMBA LA MAFUTA NI SALAMA KWA MAZINGIRA- MKURUGENZI NEMC


MRADI WA BOMBA LA MAFUTA NI SALAMA KWA MAZINGIRA- MKURUGENZI NEMC

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka ameitisha mkutano na waandishi wa habari kuhusu suala la baadhi ya wanaharakati kutoka Mataifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kupinga ujenzi wa bomba la Mafuta linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Mkoani Tanga leo tarehe 16 Mei 2022.

Akiongea na waandishi wa habari Dkt. Gwamaka ametolea ufafanuzi suala la baadhi ya wanaharakati kupinga ujenzi wa bomba hilo kwa madai ya kuwa ujenzi huo una athari kwa mazingira.Bomba hilo ambalo ujenzi wake bado unaendelea linatarajiwa kupita katika Mikoa nane na Wilaya ishirini na nne hadi kufika mwisho wa bomba hilo Chongoleani Tanga ambapo itajengwa bohari ya kuhifadhia Mafuta na miundombinu ya kujazia Mafuta kwenye Meli.

Dkt Gwamaka alisema "Baraza limehakikisha kwamba mradi huu wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki umezingatia masuala yote ya hifadhi ya mazingira kabla na wakati wa utekelezaji wake. Mradi huu ulisajiliwa na Baraza mwezi Machi 2017 takribani miaka mitano iliyopita na Kampuni ya Total East Africa Midstream ambayo ndio mwekezaji wa mradi huu uliopewa namba ya usajili 6725 kwa ajili ya mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira."

Aidha aliongeza kuwa Baraza lilihakiki andiko la tathmini kwamba linazingatia na kuweka mipango yote ya kudhibiti athari za mazingira na masuala ya kijamii pamoja na kushirikisha wadau muhimu katika mikoa na wilaya zote zinazopitiwa na bomba hili la mafuta. Pia taasisi zote za serikali na zisizo za kiserikali pamoja na wataalamu kutoka Baraza walihusika katika kupata maoni kuhusu mradi huu,ikiwemo kufanya ziara katika maeneo yote ya mradi kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 14 February 2019 na kufanya mapitio ya tathmini ya athari za mazingira kwa awamu mbili.

Awamu ya kwanza ni kikao cha kupata maoni ya wadau wote kutoka ngazi ya Taifa hadi wilaya na awamu ya pili ni kikao cha kamati ya Ushauri ya wataalamu (advisory committee) mnamo tarehe 3 April 2019 kilichohusisha wataalamu kutoka NEMC, vyuo vikuu mbalimbali, washauri elekezi pamoja na wawakilishi wa mradi,ambapo baada ya kikao hicho mradi uliidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira na kupata cheti tarehe 29 Novemba 2019.

Pamoja na hayo amesema Baraza limeridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi kwa kuwa umefuata sheria na kanuni zote za nchi zinazosimamia miradi ya maendeleo, mazingira na uwekezaji hivyo athari za mazingira zitokanazo na mradi huu zinaratibiwa kwa utaratibu husika ulioainishwa katika andiko la tathmini ya athari za mazingira.Hatua za awali za ujenzi zimehusisha kulipwa kwa fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo mradi huu unapitia na Baraza linafuatilia kwa karibu utekelezaji wa suala hilo kwa kufanya ziara eneo la Chongoleani na kujadiliana kuhusu hatua za utekelezaji kama zilivoainishwa kwenye andiko hilo.

Hivyo Dkt Gwamaka amewahakikishia watanzania kuwa" bomba hili la mafuta litaleta manufaa kiuchumi katika nchi yetu na wote walioguswa na mradi huu haswa waliohamishwa katika makazi yao, hali zao za maisha kubadilika na kuwa bora zaidi kuliko hapo awali ikiwemo ujenzi wa nyumba bora na za kisasa kwa waliohamishwa. Pamoja na kutoa ajira mbalimbali kwa watanzania". Pia amewaomba wananchi kupuuzia maneno ya wanaharakati wanaopinga ujenzi huu kwani bomba hili lina manufaa makubwa kwa nchi na Afrika Mashariki wa ujumla.