MARUFUKU UCHIMBAJI MCHANGA KATIKA MITO- Mh. ZUNGU


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Azzan Zungu amefanya ziara katika mto wa Nyakasangwe uliopo mtaa wa boko, kata ya Bunju, jijini Dar es salaam kujionea hali halisi ya uchimbaji wa mchanga katika mto huo.

Katika ziara hiyo Mhe. Zungu aliambatana na Meneja wa kanda ya Mashariki NEMC Bw. Arnold Mapinduzi pamoja na kikosi kazi cha NEMC, Bonde na Manispaa ya kinondoni.

Aidha Mh. Zungu amebaini changamoto nyingi zinazowakabili wakazi wa maeneo hayo pamoja na uharibifu wa Mazingira kutokana na uchimbaji mchanga kiholela unaofanywa na baadhi ya watu katika eneo la mto huo

“Sasa hivi tumegundua tatizo biashara hii ya uchimbaji mchanga ndani ya mito ni haramu na inaharibu Mazingira yetu, unapotoa mchanga katika mto huu bila muongozo matokeo yake maji yatahama katika njia ya asili yatakwenda kugonga nyumba za watu na yanakwenda kugonga kwenye miundombinu ya Serikali, hakuna sehemu ambayo Serikali inapata hasara kama madaraja kuanguka kutokana na watu kuharibu Mazingira katika maeneo haya ya mito” alisema Mh. Zungu

Mh. Zungu ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira imekataza kuchimba mchanga katika Mito bila ya kibali kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Mazingira. Hata hivyo ameeleza kuwa hili sio jukumu la NEMC tu kusimamia utunzaji wa mazingira bali pia sheria inatambua ngazi za halmashauri, Kata na mtaa hivyo kutosimamia Sheria ni makosa.

“Marufuku kwa mtu yeyote kuchimba mchanga katika eneo hili bila kupata muongozo kutoka kwa wataalamu wetu” alisema Mh. Zungu

Kwa upande wake Bw. Arnold Mapinduzi Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki ameeleza kuwa sheria ya Mazingira inasema mtu yoyote asifanye shughuli zozote za kudumu ikiwa ni pamoja na makazi mabondeni ndani ya mita 60, na yenyewe pia inakiukwa na tatizo limekuwa sugu

“Mhe Waziri tunaomba watu wa mipango miji, bonde, madini na kitengo cha mipango miji tukutane kama forum ili tuweza kulisimamia jambo hili kwa pamoja” alisema Bw. Mapinduzi

Hata hivyo Mh. Zungu akiwa kwenye ziara hiyo alitembelea katika mto Salasala kujionea changamoto zinazojitokeza kwa wananchi walio karibu na mto huo Mhe. Waziri amejionea mazara yaliyojitokeza kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga na kuagiza kuwa wanaojishughulisha kuchimba mchanga waache mara moja endapo watabainika hatua za kisheria zitachukuliwa.