MAKAO MAKUU YA (NEMC) RASMI KUHAMIA DODOMA




Makao Makuu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC yametangazwa rasmi kuhamia Dodoma kuanzia siku ya Alhamisi tarehe 25 ya mwezi wa nane Mwaka huu.



Tangazo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo Dkt Samuel Gwamaka alipokuwa akiongea na watumishi wake katika hafla ya pamoja ya kuagana iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa NEMC.



Amesema kwa Makao Makuu ya Ofisi za NEMC kuhamia Dodoma katika jengo la Kambarage ghorofa ya sita(6), ni kutekeleza agizo la Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha ofisi zote za Serikali pamoja na shughuli zake zinahamia katika Mji wa Serikali ambao ni Dodoma.



"Agizo hili lilipotolewa tulisuasua kidogo kwani tulikuwa tukiangalia utaratibu wa namna sahihi ya kukamilisha ofisi zetu na kuungana na Taasisi nyingine katika Mji wa Serikali, lakini pia NEMC katika kukua tumeunda Kanda ambapo kimsingi tumepanua wigo katika kutoa huduma. Lakini pia katika maisha yeyote yale kuhama ndio kukua, hivyo ni wajibu wa kila Mtumishi kuzingatia hilo." Amesema Dkt Gwamaka.



Ameongeza kuwa NEMC ni Baraza la Taifa lenye jukumu kubwa la kuhifadhi na kuyalinda Mazingira hivyo imejizatiti katika kuboresha huduma zake kwa jamii kwa kuunda Kanda Nchi nzima, ambapo kwa sasa ziko Kanda 9.



Naye Mkurugenzi wa fedha na Utawala Ndg Charles Wangwe alipokuwa akizungumza amesema kwa NEMC kuhamia Dodoma ni katika kufuata miongozo na maelekezo ya Serikali, lakini pia ni kukua katika Utumishi wa Umma wenye lengo la kuleta maendeleo katika Taifa letu.



Makao Makuu ya NEMC yatakuwa katika jengo la Kambarage ghorofa ya sita rasmi kuanzia siku ya Alhamisi tarehe 25 mwezi wa nane Mwaka huu