​KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE MAJI NA MAZINGIRA YAIPONGEZA NEMC KWA USIMAMIZI WA SHERIA YA MAZINGIRA


Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira chini ya Makamu Mwenyekiti wake Mhe. Anna lupembe (Mb) imelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Sheria ya Mazingira.

Pongezi hizo zimetolewa leo na kamati hiyo wakiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu mazingira yaliyotolewa kwa kiwanda cha kutengeneza chuma na nondo cha lodhia kilichopo Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

‘’Kiwanda hiki kilikuwa na uchafuzi mkubwa wa hewa unaotokana na mitambo kutoa moshi mwingi, hali iliyokuwa ikiathiri wakazi wa eneo husika pamoja na mazingira, lakini kwa sasa tunaona kwa macho hali ni nzuri udhibiti wa hewa chafu umefanyika, udhibiti wa kelele zitokanazo na mitambo umefanyika, udhibiti wa utupaji hovyo wa taka hatarishi umefanyika, hii maana yake ni kwamba NEMC wamefanya kazi yao kwa ufasaha zaidi na elimu ya mazingira imeenea, hongereni sana NEMC" Mhe. Anna Lupembe (Mb).

Ameongeza kuwa ni vema pia wawekezaji wakazingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa Mazingira hasa suala la ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kabla ya uendelezaji wowote ili kuepuka changamoto za kimazingira hasa ikizingatiwa utunzaji wa mazingira kwa wawekezaji kote nchini ni jambo la kuzingatiwa kwani azma ya Mhe.Rais Mama Samia ni kuendeleza uwekezaji na kutunza Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Naye waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt.Selemani Jafo alipozungumza ameishukuru kamati ya kudumu ya Bunge Maji na Mazingira kwa ziara hiyo ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa kiwanda cha Chuma na Nondo Wilayani Mkuranga na kuwataka wawekezaji wengine kuiga mfano mzuri wa utunzaji wa mazingira kutoka kwa Mwekezaji Lodhia wa kiwanda kilichopo Mkuranga.

Kadhalika Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nondo, Chuma na Plastiki Ndg. Sailesh Pandit alipokuwa akipokea maelekezo na ushauri kutoka kwa kamati ya bunge, ameahidi kuyatekeleza kwa wakati na kulinda mazingira kwa mstakabli wa maendeleo endelevu ya Taifa na pia kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania hasa wanawake ili kukuza uchumi wa viwanda.

Ziara hiyo imehudhuriwa na kamati ya maji ya bunge, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mkuranga, Menejimenti nzima ya NEMC pamoja na wadau wa mazingira