​HAYA NDIO MAAGIZO YA MAZINGIRA ALIYOYATOA WAZIRI MKUU KWA WAKUU WA MIKOA KOTE NCHINI.


Waziri mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka wakuu wa Mikoa yote Nchini kukaa na mabaraza ya biashara, wamiliki wa kumbi za starehe, katika mikoa yao ili kutafuta muafaka wa pamoja katika utekelezaji wa Sheria, Kanuni na miongozo kuhusu udhibiti wa athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango

Ametoa maelekezo hayo wakati akizindua kongamano la kujengewa uelewa kuhusu madhara yatokanayo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada, lililoandaliwa na Jumuiya Maridiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira NEMC na kufanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam(JNICC)

‘Leo kunakongamano la Kitaifa linaloratibiwa na JMAT na NEMC, wekeni mpango wa kufanya makongamano kama haya hadi katika ngazi ya Mikoa ili jamii iwe na uelewa wa pamoja kuhusu athari za viwango vya sauti vinavyozidi. Aidha toeni elimu kwa umma ili wajue viwango halisi vya sauti vinavyostahili wakati wa mchana na wakati wa usiku’ Amesema Mhe. Majaliwa

Ameongeza kuwa wakuu wa Mikoa ndio Marais katika maeneo yao, wamepewa dhamana ya kulinda wananchi katika nyanja zote ikiwemo Mazingira, hivyo niwajibu wao kukutanisha mabaraza na vikundi ili kwa pamoja kufikiwe muafaka wa udhibiti wa sauti zilizozidi viwango katika maeneo mliyokasimiwa madaraka kuyaongoza.

Aidha Mhe. Majaliwa pamoja na maelekezo hayo ya kukutana, amezielekeza idara za Mipangomiji katika Halmashauri za Wilaya kote nchini kusimamia miongozo inayotekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na maedneleo ya makazi katika upangaji wa miji na kutoa miongozo mahususi ya matumizi ya ardhi hasa utengaji wa maeneo kwa ajili ya nyumba za ibada kama wanavyotenga ya taasisi nyingine.

‘Kwa upande wa udhibiti wa sauti zilizozidi viwango Mhe.Majaliwa amesema , kila mamlaka itimize waibu wake kulingana na maelekezo yaliyomo katika muongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira utokanao na kelele na mitetemo uliotolewa na ofisi ya makamu wa Rais na kuwataka kuwa na utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa matumizi ya vibali au leseni ya shughuli au biashara wa matumizi ya leseni hizo.

.Akizungumza kuhusu wamiliki wa majengo, Waziri Mkuu amewataka kuzingatia ufanyajiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa watu wanaotumia majengo hayo, pamoja na wakazi wa jirani na majengo hayo kwa lengo la kubaini madhara kwa watumiaji wake na jamii inayozunguka.

Kadhalika Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa dini wanaoshiriki katika kongamano hilo kuendelea kuwa kielelezo na balozi wazuri wa kufikisha yale mambo mazuri yanayowasilishwa katika kongamano hilo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema madhumuni ya kongamano hilo ni kuwakutanisha pamoja viongozi wa dini na mila ili kutoa elimu ya athari za sauti zilizozidi viwango kutoka kwenye nyumba za ibada na jamii.

Ameainisha Kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015 zimeainisha viwango vinavyoruhusiwa katika maeneo ya makazi, nyumba za ibada, biashara, viwanda na hospitali kwa ajili ya jamii, mfano viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika nyumba za ibada zilizopo katika maeneo ya makazi ni dBA 60 wakati wa mchana na usiku ni dBA 40

Amesema sauti zinazozidi viwango katika nyumba za ibada zinaweza kuathiri afya za waumini na wakaazi wa maeneo ya jirani na kusababisha matatizo ya kusikia kukosa usingizi na kuathiri uwezo wa kufanya kazi pamoja na kusababisha migogoro kati ya wakazi na viongozi au waumini.

Dkt Gwamaka amesema NEMC itaendelea kusimamia kwa ukamilifu uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria na Kanuni zake kwa kuandaa semina, warsha na mikutano ili kujenga uelewa mpana zaidi kwa jamii na wadau kadiri inavyohitajika, ‘Nitoe wito kwa viongozi wa dini tushirikiane katika utekelezaji wa Sheria hizi ili kuboresha ustawi wa Mazingira yetu.

Awali katibu mkuu wa JMAT Askofu Dkt Israel Maasa alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wenzake wa dini mbalimbali nchini kwa kuendelea kushirikiana hali inayolifanya Taifa liendelee kuwa kitovu cha Amani na utulivu