​FAHAMU FURSA NACHANGAMOTO ZA TAKA NGUMU MKOA WA DAR ES SALAAM


FAHAMU FURSA NACHANGAMOTO ZA TAKA NGUMU MKOA WA DAR ES SALAAM

Takataka ni uchafu ambao unatokana na mabaki ya vitu baada ya kuzalishwa au kutumika ambao hauwezi kutumika tena bila ya kurejelezwa kwa matumizi mengine. Taka hizo huzalishwa majumbani, viwandani na maeneo ya biashara. Watu wengi huamini na kujenga dhana kuwa takataka ni uchafu ambao hauwezi kutumika tena kwa matumizi mengine hali iliyoplekea kuwa na taka nyingi kushinda uwezo wa miundo mbinu iliyopo. Aidha, jamii inakumbushwa kuwa kuna fursa nyingi zitokanazo na taka hizo.

Ili kuweza kutambua fursa zitokanazo na takataka tunatakiwa kutambua aina za takataka ambazo zinazozalishwa katika jamii yetu. Tutambue kuwa kuna aina tatu za takataka ikiwemo taka ngumu, taka maji na taka gesi.

Katika kudhibiti taka ngumu Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake imetoa mamlaka katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini kusimamia Sheria hiyo. Pamoja na Sheria hiyo kuwa wazi na kutoa mamlaka katika Halmashauri na Serikali za Mitaa kuhusu udhibiti wa taka ngumu, lakini bado kuna changamoto nyingi katika usimamizi.

Mkoa wa Dar es Salaam, kwa mfano, ni Mkoa wa kibiashara na ni Mkoa wenye watu wengi kuliko mikoa mingine yote nchini. Hali ya usafi wa jiji la Dar es Salaam hususani udhibiti wa taka ngumu ni tatizo la muda mrefu ambalo lina changamoto nyingi.

Jamii ya wakazi wa Dar es Salaam miongoni mwao wamekuwa na tabia ya utupaji wa taka katika maeneo yasiyo rasmi, tabia hii imechangia kwa kiasi kikubwa jiji kuwa chafu na kusababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira katika jamii ikiwemo magonjwa kama vile kipindupindu, kuhara, kutapika, kansa, pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji na mafuriko.

FURSA ZINAZOTOKANA NA TAKA NGUMU

Kama tunavyojua kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Mkoa wa kibiashara ambao una fursa nyingi ya upatikanaji wa viwanda ndani yake, ni Mkoa wenye watu wengi kutokana na hili taka nyingi kutoka majumbani na katika shughuli za kijamii ikiwemo kilimo, ofisini, viwandani, masoko, madukani, taasisi za kiserikali huzalishwa. Taka hizo nyingi hutupwa kwenye madampo na nyingine huchomwa kwenye maeneo ya makazi. Wananchi wanatakiwa watambue kuwa sio kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kiishie kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kubwa ya kujipatia kipato na kuweza kuendesha maisha yao.

Taka ngumu huweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa mfano mabaki ya chakula huweza kutumika kulishia mifugo kama paka, mbwa na nguruwe. Aidha, mabaki hayo yanaweza kutumika kuzalisha gesi na mbolea. Kwa upande mwingine taka za plastiki kama chupa na ndoo vinaweza kutumika kwa ajili ya kuwekea maua au kuuza katika viwanda vinavyoweza kurejeleza. Taka za chuma chakavu au nyaya za umeme zilizochakaa zinaweza kukusanywa pamoja na kuuzwa katika viwanda husika.

Umuhimu wa kutumia takataka zinazozalishwa kwa matumizi mengine umezingatiwa kwa kiasi kikubwa na Baraza la Taifa ka Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Hivi karibuni kwa mfano, Mkurugezi Mkuu NEMC, Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka alisema kuwa takataka isiwe kero bali iwe ni mojawapo ya chanzo cha kujipatia kipato na kuweza kupunguza mzigo katika madampo yetu. Ameeleza kuwa ili kuweza kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani zinatakiwa kutenganishwa na sio kuchanganywa. Endapo zitachanganywa zitasababisha kushindwa kuchambuliwaa na kuweka ugumu wa uteketezaji katika madampo yetu.

Dkt. Gwamaka alieleza kuwa Sheria ya Mazingira imewapa mamlaka Halmashauri, Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia zoezi la ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa taka hizo. Ingawa NEMC imetajwa kwenye kanuni lakini wasimamizi wakuu ni Halmashauri, Manispaa na Serikali za Mitaa.

Aliendelea kusema kuwa pia Sheria ya Mazingira imemtambua na kumpa nguvu mkaguzi wa mazingira ambaye anateuliwa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira. Wakaguzi hao wapo wilaya na mikoa yote kwa ajili ya kusimamia shuguli za utunzaji wa mazingira.

Dkt. Gwamaka alisema kuwa utupaji wa taka hovyo katika maeneo mbalimbali mkoani wa Dar es Salaam umekithiri hivyo kunafanyika jitihada mbalimbali ya kuhakikisha Maafisa Mazingira wa Halmashauri na watendaji wa Serikali ya Mitaa wanapewa elimu ya mazingira ili kupanua uelewa, kwani kero kubwa zinazotoka kwa jamii yetu ni kutokana na kutoelewa Sheria ya Mazingira na Kanuni mbalimbali zinazo ratibu utendaji.

Katika kutafuta msingi wa kuweza kutatua changamoto na malalamiko yanayoletwa na wananchi, NEMC iliandaa warsha ya kutoa elimu kwa viongozi na watendaji wa Kata na Mtaa katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kupata suluhisho ili kuweka ustawi wa mazingira katika maeneo husika. Pia lengo la warsha hiyo ni kuwaelekeza majukumu ya kisheria na kiutendaji pamoja na kuweka mahusiano ya karibu na Baraza katika kutatua changamoto za kimazingira katikajamii.

Umuhimu wa elimu kwa jamii ni kutokana na NEMC kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya changamoto wanazopata katika ukusanyaji wa taka kuna baadhi ya maeneo wanakaa na taka kwa muda mrefu bila ya kukusaywa na jamii ikifahamu kua suala la ukusayaji wa taka za majumbani ni la NEMC. Sheria imetaja NEMC kuwa msimamizi lakini msimamizi mkuu wa taka hizo ni Halmashauri, Manispaa na Serikali za Mitaa katika mikoa. Hivyo kuweza kupunguza changamoto katika ukusanyaji Mwananchi unatakiwa kuzitegaisha taka hizo kabla ya kwenda kutupwa kweye madampo kwa ajili ya uteketezaji. Tumia fursa za taka kujiongezea kipato.