‚ÄčELIMU YA UDHIBITI WA KELELE NA MITETEMO YAWA KIVUTIO BANDA LA NEMC


Elimu ya Udhibiti wa kelele na mitetemo kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake, yavutia wadau wengi hasa ikizingatiwa ndio changamoto kubwa inayoikumba jamii kwa sasa.

Elimu hiyo iliyohusisha tafsiri ya kawaida ya kelele, vyanzo vya kelele, athari za kelele pamoja na njia za kudhibiti sauti zilizozidi viwango na mitetemo imewafurahisha wengi hasa wale waliozungukwa na nyumba za ibada, viwanda na kumbi za burudani.

Akizungumza na wadau hao Bi.Furaha Benjamin ambaye ni Afisa Mazingira Kanda ya Nyanda za Juu kusini amesema elimu hii ni vizuri kuifahamu kwa usahihi ili mmiliki wa kumbi au kiwanda au wale waliozungukwa na vyanzo vya kelele wajue namna sahihi ya kudhibiti kwa mstakabali wa Afya.

Bi Furaha amezitaja athari za sauti zilizozidi viwango kuwa ni wanafunzi kushindwa kujisomea, husababisha ulemavu wa usikivu, kuharibu mahusiano ya jamii, kukosa usingizi, huathiri mawasiliano pamoja na kukosesha wagonjwa na wazee usingizi.

Ameziainisha njia za kuzuia kelele kuwa ni matumizi sahihi ya ardhi kwa ajili ya shughuli zinazozalisha kelele, wamiliki wa biashara kupata vibali kutoka mamlaka husika pamoja na matumizi ya vidhibiti kelele.

Wananchi na wadau wengi waliomiminika katika Banda la NEMC maonesho ya Nanenane Mjini Mbeya, wamefurahishwa na elimu ya udhibiti wa kelele na mitetemo inayotolewa mahali hapo