ELIMU YA MAZINGIRA KIVUTIO MKUTANO WA AMECEA


ELIMU YA MAZINGIRA KIVUTIO MKUTANO WA AMECEA.

Elimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira inayotolewa na NEMC imeonekana kuwavutia wengi katika Mkutano wa 20 wa AMECEA uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere Jijini Dar es salaam.

Elimu hiyo iliyohusisha tathmini ya athari kwa mazingira, utekelezaji na uzingatiaji wa mazingira, masuala ya tafiti kwenye mazingira, pamoja na huduma za kisheria imetolewa kwa Mataifa tisa yaliyoshiriki kwa lengo la kujadiliana athari za maendeleo katika mabadiliko ya tabia Nchi.

Akiongea na vyombo vya habari, Askofu Flavian Kassala wa Jimbo la Geita amesema kazi inayofanywa na NEMC kuhusiana na mazingira ni muhimu sana kwani imerahisisha ufuatiliaji na uzingatiaji wa sheria katika utekelezaji wa jukimu lake kuu la utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Amesema elimu ya mazingira yapaswa kuzingatiwa sana kwani ndio msingi imara wa upangaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kuzingatia athari zinazoweza kutokea katika suala zima la mabadiliko ya tabia Nchi.

Akielimisha Umma huo kipengele cha tathmini ya athari kwa mzingira mtaalam kutoka NEMC Bi. Suzan Chawe amesema ni vizuri kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa kutoka mamlaka husika katika uandaaji wa ripoti za TAM kwa miradi ya maendeleo ili kuepukana na changamoto za kimazingira zinazoweza kutokea kubwa ikiwa mabadiliko ya tabia Nchi.

Nchi zilizoshiriki katika Mkutano huo ni Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan, Afrika ya Kusini, Uganda, Zambia na Tanzania ambayo kwa mwaka 2022 ndio mwenyeji.

Imeandaliwa na

Kitengo Cha Mawasiliano

NEMC