NEMC yaomba wananchi mipakani kuchukia magendo ya mifuko ya plastiki


Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa, wakati wa ziara ya siku moja ya kufuatilia na kutathiminiu utekelezaji amri ya serikali ya kupiga marufuku matumitizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki na ustawi wa biashara ya mifuko mbadala, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC,Dk.Samuel Gwamaka amesema Sheria ya Mazingira ya 2004 na Kanuni zake lazima zifatwe ili kulinda mazingira ya Tanzania.

“Ulinzi wa mipakani ni muhimu uhimalishwe ili kuzuia kuingiza kwa magendo wa mifuko kutoka nje. Tunatarajia wananchi washio maeneo ya mpakani mchukie biashara ya magendo ya aina hii na mfichue wanaofanya biashara hii kwa mamlaka husika, maana mifuko ya plastiki na vifungashio vinavyoingizwa nchini kwa njia ya magendo vitayadhuru mazingira na kuua soko la wazalishaji wa ndani,” amesema Dk.Gwamaka

Amesema wananchi washirikiane na vikosi kazi vya mazingira vilivyopo katika kila mkoa kuzuia mifuko ya plastiki kuingia na kutumika nchini, na kuviuomba vikosi kazi kuendeleza elimu juu ya umuhimu wa kutumia mifuko mbadala katika utunzaji wa mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae.

“Matumizi ya mifuko mbadala yenye kiwango cha GSM70 yanahimizwa kwa sababu yanalenga kulinda wazalishaji wa ndani na pia kwenda sambamba na azma ya serikali ya awamu ya tano ya ujenzi wa uchumi wakati na viwanda. Hivyo ni lazima tuilinde mipaka yetu na kuzuia biashara ya magendo ya mifuko ya plastiki kwani biashara hiyo itazorotesha soko la ndani la mifuko mbadala,” ameeleza Dk.Gwamaka.

Akigusia azma ya NEMC ya kuhakikisha utekelezaji wa katazo la serikali unafanyika kwa utaratibu mzuri, Dr Gwamaka amesema baraza limetoa mwezi mmoja kuhakikisha matumizi ,uzalishaji na usambazaji wa vifungashio vya plastiki vinasitishwa ili vifungashio mbadala vitumike kwa lengo la kulinda mazingira.

Dk Gwamama amesema vifungashio mbadala vipo lakini imeonekana kwamba watu wanachagua kutumia plastiki kwa kutaka urahisi wa kufanya kazi zao, na kuwaomba wananchi waelewe kwamba Sheria ya Mazingira na Kanuni zake vitatumika kikamilifu ili kuzua matumizi ya plastiki aina yote ikiwamo matumizi tubing katika kufunga bidhaa, hasa vyakula, ili kulinda afya ya mlaji.


Amesema vikosi kazi vya mazingira vitaendelea kutoa elimu ya matumizi ya vifungashio na vibebeo ili kuwajengea uelewa wananchi, na kuongeza usimamizi wa utunzaji wa mazingira na katazo la plastiki ndani ya jamii.

Bi.Jestina Mwalupengo, mkazi wa Tunduma, amesema matumizi ya mifuko ya plastiki bado yapo katika eneo lao na kudai kwamba mifuko hiyo inatoka nchi jirani.

“Tutaendelea kuhamasishana wenyewe ili kuzuia mifuko isiingizwe nchini. Matokeo ya mifuko iliyopigwa marufuku tunayaona hapa. Ni mazuri kwani yamefanya mazingira kuwa salama tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya katazo,” amesema Bi.Mwalupengo

Bw.Lasmos Muyinga, ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo Tunduma mjini, ameipongeza Serikali kwa kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki nchini na kueleza kwamba hali ya mazingira ilikuwa mbaya sana kutokana na mifuko hiyo kuzagaa ovyo. “Tatizo mifuko hii haiozi,”ameeleza..