Wananchi walalamikia kiwanda cha Axel - Bagamoyo


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu amefanya ziara katika kiwanda cha Axel Chemical Ltd, kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani ili kubaini uhalali na uendeshwaji wa kiwanda hicho, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau wa mazingira.

Waziri Zungu akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Kawawa, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka na watumishi wengine, amegundua jina la kiwanda ni Exel Chemical huku bidhaa zikienda kwa jina la Watercraft jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha Waziri Zungu ametoa rai kwa uongozi mjini Bagamoyo kufanya mapitio ya viwanda vyote ili kutambua endapo vinaendeshwa kihalali.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Kawawa amewataka wawekezaji kufuata taratibu za kisheria ili kuepusha usumbufu na athari kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Samwel Gwamaka amesema baada ya ukaguzi walibaini uwepo wa kelele pamoja na vumbi lililokithiri katika kiwanda hicho jambo ambalo ni tishio kwa afya za wakazi wa eneo hilo.

Hatahivyo uchunguzi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na usajili, ulipaji wa kodi na tuhuma mbalimbali zilizotolewa na wananchi wa eneo hilo.