ADA NA TOZO ZA MAZINGIRA


ADA NA TOZO ZA MAZINGIRA

Utangulizi

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na Kanuni ya Ada na Tozo za Mazingira ya 2021. Wadau mbalimbali wa Mazingira wameelimishwa kuhusu wajibu wa kuhifadhi na kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kulipa ada na tozo za mazingira. Zoezi la uelimishaji limehusisha Ofisi zote za Baraza ikiwa ni pamoja na Makao Makuu na Ofisi za Kanda tisa (9).

Ikumbukwe kuwa Baraza linajiendesha katika kusimamia majukumu yake ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa kutumia fedha zitokanazo na Ada na Tozo mbalimbali za Mazingira. Hii ikiwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004. Tozo zitumikazo kwa sasa zimeainishwa katika Kanuni ya Ada na Tozo za Mazingira ya mwaka 2021 katika toleo la Serikali namba 387 lililochapishwa tarehe 14/05/2021.Tozo hizo za Mazingira zinahusisha shughuli zote zinazoendelea na zinazotarajia kuanza kama ambavyo Kanuni imeanisha.

Ada na tozo ya mazingira maana yake ni kiwango cha pesa kinacholipwa au kinachotozwa na Baraza kwa ajili ya kuwezesha kufanya mapitio ya Tathmini za athari kwa Mazingira, na vilevile ufuatiliaji na uhakiki wa mazingira kama ilivyoainishwa katika sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Ada hizi hulipwa na (miradi yote iliyoanishwa kwenye kanuni pamoja watalamu washauri wa mazingira) kila mwaka wa fedha wa Serikali. Tozo zimeainisha aina ya miradi na viwango vyake. Aidha, tozo zingine zinatozwa kutokana na kutozingatia viwango na kanuni za mazingira, pamoja na vibali maalumu vitolewavyo na Baraza.

Baraza limepewa jukumu na mamlaka kisheria kufuatilia na kuhakiki uzingatiaji wa viwango vya mazingira kwa miradi yote inayoanzishwa nchini. Katika kutekeleza jukumu na mamlaka hayo inategemeana na rasilimali watu na fedha. Mwanzoni Baraza lilitegemea sana ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo na ruzuku kidogo kutoka Serikalini ili kutekeleza majukumu yake. Mwaka 2008, Bunge liliridhia kanuni za ada na tozo za mazingira ilianzishwa ikiainisha miradi yote inayochafua /kuharibu mazingira kulipa ada na tozo za mazingira kulingana na aina ya mradi. Kwa sasa mchakato huu unasimamiwa na Kanuni ya Tozo za Mazingira ya Mwaka 2021 (Environmental Management (Fees and Charges) Regulations, 2021)

Matakwa ya Kisheria Kuhusu Ada na Tozo

Viwango vya Tozo vimeainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Kifungu Na 230(2) (b) iliyotengeneza Kanuni ya Ada na Tozo ya mwaka 2021. Hii inahusisha Ada na Tozo za mwaka, Usajili wa Miradi, Gharama za mapitio ya miradi na faini (penalty). Aidha, Sehemu ya Sita ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 yenye Kifungu cha 81 hadi cha 103 inaelekeza kila shughuli ya maendeleo ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa Mazingira na inatoa ufafanuzi wa hatua za kufuata. Vilevile Sheria imeainisha jukumu la mwekezaji la gharama za kulipia kwa ajili ya mapitio ya Taarifa za Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).

Kwa mara ya kwanza Kanuni ya Tozo ilianzishwa mwaka 2008 na ilianza kutumika mwaka wa fedha wa 2012/2013. Baraza linafahamisha kuwa Kanuni za Tozo zimefanyiwa marejeo mara kadhaa tangu kanuni za tozo kuundwa mwaka 2008. Kanuni hizo zilifanyiwa mabadiliko mwaka 2016 na Mwaka 2018, Mwaka 2019 na Mwaka 2021 ikiwa ni katika mustakabali wa kutekeleza Mwongozo wa Serkali wa kuboresha Mazingira ya Uwekezaji nchini (Blue Print on Regulatory Reform to Improve Business Environment in Tanzania). Hata hivyo, Kanuni za Ada na Tozo za mwaka 2019 ziliboreshwa kufuatia mabadiliko yaliyofanyika kwenye Kanuni za Taka Hatarishi za Mwaka 2021. Viwango vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Ada na Tozo zilitakiwa kuwiana na shughuli zinazofanyika kwenye usimamizi wa taka hatarishi ikiwa ni pamoja na ukusanyaji, usafirishaji na utunzaji.

Gharama za Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM)

Baraza kwa nyakati tofauti limelazimu kutoa ufafanuzi juu ya aina mbalimbali za tozo kwani wadau wamekuwa wakishindwa kutenganisha gharama za mapitio zinazolipwa NEMC na zile za ufanyaji TAM na uandaaji wa andiko zinazitakiwa kulipwa kwa mtaalam elekezi. Gharama za TAM ziko kwenye makundi makuu mawili: 1) Gharama za moja kwa moja za mradi na 2) Gharama za mapitio ya mradi (ada za NEMC kama zilivyoainishwa kwenye Kanuni).

Gharama za mradi zinategemea mambo kadhaa ikijumuisha: 1) Eneo ambapo mradi upo (makazi ya watu, kwenye hifadhi, kwenye mkondo au chanzo cha maji; 2) Ukubwa na shughuli mbalimbali zinazohusu mradi; 3) Changamoto za kimazingira na kijamii zinazoweza kujitokeza kutokana na uanzishaji wa mradi; 4) Aina ya mradi (mgodi, kiwanda cha utengenezejia wa kemikali na 5) Taswira ya mradi kwa mamlaka husika na jamii inayozunguka eneo la mradi kwa ujumla

Gharama za moja kwa moja za TAM kwa Wataalamu Elekezi ni zile gharama za mchakato mzima wa uandaaji wa andiko la TAM ambazo hulipwa moja kwa moja kwa mtaalamu elekezi. Gharama hizi zinajumuisha mambo kadhaa kulingana na mchakato ulivyo. Mara nyingi gharama hizi hujumuisha gharama za utaalamu wa ufanyaji tathmini, uchukuaji na upimaji wa sampuli na uandaaji wa andiko na pia gharama za usafiri na malazi ukusanyaji wa taarifa mbalimbali. Gharama za TAM ni suala la makubaliano baina ya mteja na mtaalam TAM.

Muda wa Ulipaji Ada na Tozo za Mazingira

Tozo za Mazingira za Mwaka hutakiwa kulipwa katika kipindi cha kuanzia tarehe 1/7 hadi Tarehe 31/12 ya kila mwaka wa fedha kwa mujibu wa sheria. Aidha ucheleweshaji wa ulipaji wa tozo baada ya tarehe 31/12, zitalipwa na penati ya 5% kwa kila mwezi ambao umepitishwa. Kuhusu malipo ya mapitio ya Tathmini za Athari za Mazingira na Ukaguzi, Baraza litatoa Hati ya Madai (Invoice) na Kumbukumbu Namba ya Malipo (Control Number) inayoonesha kiwango cha gharama za mapitio ya tathmini kinachotakiwa kulipwa kutokana na Kanuni ya ada na Tozo ya Mwaka 2021. Kiasi hicho kinatakiwa kilipwe kabla au wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Tathmini ya Athari ya Mazingira au Taarifa ya Ukaguzi wa Mazingira. Gharama hizo zinatofautiana kulingana na mradi husika.

Vilevile wamiliki wa miradi wanatakiwa kutoa taarifa Baraza pale ambapo miradi yao itakuwa imefikia ukomo wa utekelezaji ili Baraza liweze kujiridhisha kama wametekeleza Sheria ya mazingira kama vile kulipa Ada na Tozo mbalimbali pamoja na kuhakikisha, matakwa ya kurekebisha hali ya mazingira yamezingatiwa katika uhitimishaji wa utekelezaji wa miradi.

Huduma kutoka katika Ofisi za Kanda

Katika kuhakikisha huduma kwa jamii zimesogezwa, Baraza limeanzisha ofisi za kanda. Hatua hii ni mahsusi kurahisisha utendaji kazi wa Baraza hususani masuala ya Tathimini za Athari za mazingira, Ukaguzi pamoja na utoaji elimu. Aidha, Ofisi za Kanda zimekuwa na mchango mkubwa katika jitihada zinazofanywa na Baraza za ukusanyaji Ada na Tozo za mazingira. Hadi sasa Baraza lina jumla ya Ofisi za Kanda tisa (9) ambazo zinatoa huduma za mazingira kwa jamii.

Hitimisho

Kulipia tozo ni takwa mojawapo la kisheria katika uzingatiaji na utekelezaji wa sheria. Hivyo, Baraza limeendelea kutoa elimu kwa njia ya radio, televisheni, magazaeti na kwenye tovuti yake kuwakumbusha wawekezaji kukamilisha michakato ya EIA na EA na kuwakumbusha wawekezaji kuhakikisha wanakidhi matakwa ya kisheria ikiwa ni pamoja na kusajili miradi mipya kwa ajili ya TAM na miradi iliyokuwepo kwa ajili ya Tathmini ya Ukaguzi wa Mazingira. Hii pia ikiambatana na ulipaji wa tozo husika. Aidha, Baraza limeboresha Kanzidata ya wadaiwa na wadau wanaopaswa gharama za mapitio ya TAM na Tayari NEMC imejiunga na Mfumo wa malipo. Serikalini GEPG na hii inasadia katika kutambua wenye miradi ambao wanakuwa hawajalipia tozo husika.

Baraza linasisitiza kuwa lengo kuu la Tozo za mazingira ni kusaidia watumiaji wa mazingira kuona thamani halisi ya mazingira anayoyatumia na faida anayoipata kutoka kwenye mazingira. Ada na tozo za mazingira ni dhamana ambayo Mchafuzi au mharibifu wa mazingira anatakiwa alipie gharama za uchafuzi katika mazingira (Polluter Pay Principle) inayomtaka kulipia anayechafua mazingira ili pesa inayopatikana iweze kusaidia wengine ambao hawachafui mazingira.Vilevile fedha inayopatikana kwenye tozo inasaidia Baraza kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja kusimamia mazingira vizuri ili yaweze kudumu na kuwa salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.