𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈 𝐌𝐊𝐔𝐓𝐀𝐍𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐈𝐊𝐀𝐍𝐃𝐀 𝐍𝐂𝐇𝐈𝐍𝐈 𝐆𝐇𝐀𝐍𝐀 𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐃𝐇𝐈𝐁𝐈𝐓𝐈 𝐓𝐀𝐊𝐀 𝐙𝐈𝐍𝐀𝐙𝐎𝐙𝐀𝐋𝐈𝐒𝐇𝐖𝐀 𝐕𝐈𝐖𝐀𝐍𝐃𝐀𝐍𝐈


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware Semesi ameshiriki Mkutano wa Kikanda wa Kudhibiti Taka zinazozalishwa viwandani ikiwa ni pamoja na kutathmini mifumo endelevu ya urejelezaji kwa lengo la kutumia taka kama malighafi au nishati ambapo matumizi ya jinsi hiyo yatapunguza kwa kiasi kikubwa taka zinazokwenda kwenye mazingira.

Mkutano huo wa siku moja umefanyika Tarehe 30 Julai, 2024 Jijini Accra nchini Ghana na umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha Sayansi na Mazingira (Center for Science and Environment), India na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (Environmental Protection Authority), Ghana.

Mkutano huo unashirikisha taasisi za usimamizi wa mazingira kutoka nchi za Ghana, Kenya, Nigeria, na Tanzania pamoja na wadau wa maendeleo kama vile Shirika la Maendeleo la Sweden (Swedish International Development Agency) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) pamoja na Asasi za kiraia kutoka nchi za Ghana na Kenya.

Aidha, kwenye Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu ameambatana Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan H. Jangu.

Mkutano huu ni mahsusi katika kupatia ufumbuzi tatizo la taka za viwandani linalokuwa kila siku kufuatia ukuaji wa viwanda duniani wenye kusababisha uzalishaji wa taka zenye sifa mbalimbali.

Baadhi ya taka zinazozalishwa viwandani pamoja na sifa ya kuwa zenye sumu hutupwa ovyo hivyo kuhatarisha maisha ya baiandamu na viumbe wengine.

Matarajio ya Baraza ni kuwa wenye viwanda wangekuwa na hiari na utayari wa kuchukua dhamana ya kusimamia taka wanazozizalisha na kuzitumia tena kama malighani au kuhakikisha zinaharibiwa kwa mifumo inayokubalika. Mara nyingi taka hizo hutupwa ovyo na hivyo serikali na taasisi zake kutumia rasilimali fedha kidogo kutatua changamoto hizo.

Mkutano huo pia umelenga kukumbushana juu ya haja ya kuwa na mifumo sahihi ya kupunguza uzalishaji wa taka viwandani hivyo kuleta tija kwenye shughuli za viwanda.

Ushiriki kwenye Mkutano huo wa Baraza ni mwendelezo wa mashirikiano kati yake na Kituo cha Sayansi na Mazingira ambayo yamedumu kwa takribani miaka saba sasa. Taasisi hizo mbili zina makubaliano ya mashirikiano katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo kwa mafunzo na kutembelea nchi nyingine; kushiriki katika maboresho ya mikakati, kanuni na miongozo ya usimamizi wa mazingira; kufanya tafiti kuandaa maandiko ya miradi kwa lengo la kuboresha hali ya mazingira nchini.