KANDA YA MANGHARIBI

  1. UTANGULIZI

Kanda ya Magharibi ni miongoni mwa kanda kumi na tatu (13) za Baraza zilizopo nchini. Kanda hii inahudumia jumla ya mikoa mitatu ambayo ni Kigoma, Katavi na Tabora na ilianzishwa rasmi tarehe 20 Agosti 2019. Kuanzishwa kwa kanda hii ilikuwa kuhakikisha dhima ya Baraza inatekelezeka kwa ufanisi zaidi hususani katika kutimiza majukumu yake kupitia kanda na kutoa huduma za kimazingira karibu zaidi na jamii.

  1. ENEO LA KANDA

Kanda ya Magharibi ina eneo la kilomita za mraba 168,753 ikiwa ni sawa na takribani asilimia 17.9 ya eneo lote la Nchi. Kanda hii inahudumia mikoa mitatu kama ilivyelezwa hapo awali yenye jumla ya Wilaya 16 na Halmashauri 21 kama ifuatavyo:-

  1. Mkoa wa Kigoma. Mkoa huu una jumla ya Wilaya 6 na Halmashauri 8. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Kigoma, Kasulu, Buhigwe, Kibondo, Kakonko na Uvinza. Kwa upande wa Halmashauri, Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.

  1. Mkoa wa Katavi. Mkoa huu una jumla ya Wilaya 3 na Halmashauri 5. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Mpanda, Mlele na Tanganyika. Kwa upande wa Halmashauri, Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo zilizopo katika Wilaya ya Mpanda, Halmashauri za Wilaya ya Mlele na Mpimbwe zilizopo katika Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika iliyopo katika Wilaya ya Tanganyika.

  1. Mkoa wa Tabora. Mkoa huu una jumla ya Wilaya 7 na Halmashauri 8. Wilaya zilizopo katika mkoa huu ni Tabora, Igunga, Kaliua, Urambo, Nzega, Sikonge na Uyui. Kwa upande wa Halmashauri, Halmashauri zilizopo katika mkoa huu ni Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Halmashauri ya Mji wa Nzega, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

  1. MIPAKA YA KANDA

Kanda ya Magharibi inapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) upande wa Magharibi na Burundi upande wa Kaskazini Magharibi. Kwa upande wa Kaskazini, Kanda ya Magharibi inapakana na Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi (Mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga) ambapo kwa Mashariki kuna Kanda ya Kati (Mkoa wa Singida) na upande wa Kusini kuna Kanda ya Nyanda za juu Kusini (Mikoa ya Rukwa na Mbeya).

  1. MAJUKUMU YA KANDA

NEMC Kanda ya Magharibi ilianzishwa kwa madhumuni ya kutelekeza majukumu na huduma za Baraza karibu na jamii za mikoa iliyo ndani ya kanda kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu. Hivyo, Kanda hutekeleza majukumu yafuatayo: -

  1. Kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) au Ukaguzi wa Mazingira (Kuratibu, kufanya mapitio ya ripoti za TAM au Ukaguzi wa Mazingira kutoka kwa wenye miradi na kufuatilia utekelezaji wake) kwa mujibu wa sheria ili kupata vyeti stahiki.

  2. Kutekeleza shughuli za uzingatiaji na utekelezaji (compliance and enforcement) wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

  3. Kutoa ushauri wa kitaalam kwa mamlaka mbalimbali za serikali zilizopo katika kanda kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira na kusaidia taasisi na asasi mbali mbali zinazoshughulika na usimamizi wa maliasili na mazingira.

  4. Kuendesha programu za utoaji wa Elimu ya Mazingira kwa umma kupitia vyombo vya Habari na matukio mbalimbali ya Kitaifa.

  5. Kushughulikia Malalamiko, Matukio na Maoni mbalimbali ya Jamii yanayohusu Mazingira.

  6. Kuendesha na kuratibu tafiti mbalimbali za usimamizi wa mazingira

  7. Kufanya shughuli nyingine zozote kwa maagizo ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza au Waziri Mwenye dhamana ya Mazingira nchini.

  1. VIVUTIO VILIVYOKO KATIKA KANDA

Kanda ya Magharibi imebarikiwa kuwa na maeneo ya mifumo Ikolojia nyeti na maeneo ya kiutamaduni yenye umuhimu kitaifa na kimataifa. Maeneo haya pamoja na:-

  1. Ziwa Tanganyika

  2. Mito muhimu mitatu (Mto Malagarasi, Mto Ugalla na Mto Katuma)

  3. Hifadhi 3 za Taifa (Mahale, Gombe na Katavi)

  4. Hifadhi hai 1 (Gombe Masito Ugalla)

  5. Bonde Oevu la Malagarasi – Moyowosi

  6. Misitu mbalimbali ya Hifadhi

  7. Makumbusho ya Dkt Livingstone yaliyoko Ujiji (Kigoma) na Kwihara (Tabora)

  1. MAWASILIANO (MAHALI OFISI ZA KANDA ZILIPO)

Makao makuu ya Kanda ya Magharibi yako katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika Mkoa wa Kigoma. Mawasiliano ya Kanda ni kama ifuatayo: -

Meneja wa Kanda (Bw Edgar Mgila - 0713566367)