KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
UTANGULIZI
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni moja kati ya kanda 13 za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inayosimamia Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Njombe. Kanda hii ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na jukumu la kutoa huduma katika mikoa sita ya Mbeya, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Iringa. Hata hivyo, kutokana na kukua kwa huduma za Baraza, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ilibadilishiwa eneo la kiutendaji mwezi Julai, 2023 kwa kuhamisha Mkoa wa Iringa na Katavi na kujumuisha Mkoa wa Songwe ambao umemegwa kutoka mkoa wa Mbeya mwaka 2016. Hivyo, kwa sasa Kanda inasimamia eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 106,688.
OFISI ILIPO
Ofisi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ipo katika Jiji la Mbeya, katika jengo la NHIF, ghorofa ya pili.
TASWIRA YA KANDA
Kanda hii inahudumia wakazi wapatao 4,407,933 kulingana na Sensa ya Mwaka 2022, inasimama kama eneo lenye upekee usio na mfano nchini Tanzania. Umashuhuri wake unatokana na utajiri wa rasilimali za kijiografia, kibiolojia, hali ya hewa na nafasi yake muhimu kiuchumi na kimkakati. Uzuri wake wa asili, ardhi yenye rutuba na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali na kuwezesha Mikoa katika Kanda hii kuwa miongoni mwa mikoa muhimu inaochangia pakubwa katika usalama wa chakula nchini, biashara ya kimataifa na uhifadhi wa viumbe hai. Moja ya sifa bainifu za kipekee za Kanda hii ni jiolojia na hali ya hewa yake. Kijiolojia, eneo kubwa linatawaliwa na safu za milima mikubwa na vilima vinavyounda sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Milima hii inajumuisha Milima ya Livingstone, Kipengere na Mlima Rungwe. Aidha, kanda hii imebarikiwa kuzungukwa na Maziwa Makuu matatu: Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa. Uwepo wa Maziwa haya makubwa unatoa fursa za kipekee katika sekta za uvuvi, usafirishaji na utalii wa fukwe. Katika sekta ya utalii, Kanda inajivunia vivutio vya kipekee kama vile Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, inayofahamika sana kama 'Bustani ya Mungu' kwa maua yake adimu na mandhari mazuri ya milima, mapolo,oko yam aji katika mikoa yote ya Kanda. Hali hii inaifanya kanda kuwa kivutio kikuu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
NGUVU YA KANDA
Kanda ya Nyanda za juu kusini inasifika kwa uwepo wa misitu mikubwa ya biashara inayosaidia katika uzalishaji wa mbao nchini. Ufugaji wa wanyama pia unafanywa kwa kiwango kikubwa katika maeneo mbalimbali, ukichangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa bidhaa za nyama na maziwa, ardhi yenye rutuba na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali na kuwezesha Mikoa katika Kanda hii kuwa miongoni mwa mikoa muhimu inaochangia pakubwa katika usalama wa chakula nchini. Kanda hii inashikilia fursa za kipekee katika sekta ya madini kutokana na uwepo wa dhahabu, makaa ya mawe na madini ya ardhi adimu (rare earth minerals). La kipekee zaidi ni uwepo wa rasilimali ya Joto Ardhi (Geothermal), hasa katika maeneo kama Kiejo-Mbaka, Mbeya, ambayo inalenga kusaidia kuzalisha umeme na kuongeza uhakika wa nishati nchini. Kimkakati, Kanda hii ndiyo njia kuu ya barabara na reli (TAZARA) inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Zambia na Malawi. Hii inafanya Jiji la Mbeya na mipaka ya Tunduma na Kasumulu kuwa vituo muhimu vya biashara ya kimataifa na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati. Kuwepo kwa viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao ya biashara kama chai na kahawa huchochea zaidi uchumi wa ndani.
Licha ya utajiri wake, kanda hii inakabiliwa na mabadiliko ya kimazingira yanayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuathiri mifumo muhimu ya kiikolojia. Shughuli za kilimo haswa umwagiliaji na kilimo holela, ufugaji, pamoja na ongezeko la watu, zinasababisha uvamizi na uharibifu wa maeneo ya vyanzo vya maji na kingo za mito inayoingia kwenye Maziwa makuu. Hili linaathiri upatikanaji wa maji na kusababisha kukauka kwa baadhi ya mito na maziwa. Aidha, uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini na viwanda unaweza kusababisha uchafuzi wa maji na hewa na pia upanuzi wa kilimo na ufugaji, pamoja na utegemezi wa kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati, unasababisha ukataji miti hovyo. Hii inasababisha mmomonyoko wa udongo, kupungua kwa rutuba na kuharibu makazi asilia (habitats) ya viumbe hai, hasa katika maeneo ya milima na misitu. Mabadiliko ya kimataifa ya tabianchi yanajidhihirisha kwa ukame mrefu na mvua zisizotabirika au mvua kubwa zinazoleta mafuriko. Hali hizi zinatishia mazao, mifugo na miundombinu, na kuongeza uhitaji wa usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na ardhi ili kukabiliana na athari hizi. Usimamizi wa kimazingira unahitajika ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa njia endelevu na kulinda mifumo yake ya kiekolojia isiharibiwe.
MAJUKUMU YA KANDA
- Ofisi ya Kanda inamwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika kutekeleza Sheria ya Mazingira Sura 191. Majukumu mahsusi ni pamoja na:
- Kuratibu mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi mbalimbali kukuza uelewa kuhusu sheria ya mazingira na kanuni zake kwa wadau
- Kuhakikisha uzingatiaji na utekelezaji wa sheria ya mazingira na kanuni zake
- Kupokea na kushughulikia malalamiko na matukio yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira
- Kufanya tafiti za mazingira na uchunguzi katika maeneo ya mfumo ikolojia wa milima vilima, mabonde, mito na maziwa
- Kupokea na kusimamia michakato mbalimbali ya vibali ikiwa ni pamoja na vibali vya taka hatarishi
- Kuhakikisha changamoto za mazingira zinapatiwa ufumbuzi kwa njia ya tafiti na uanzishwaji wa miradi ya kimazingira
- Uratibu wa shughuli za mazingira kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kisekta/Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na wadau mbalimbali katika maeneo ya kanda
- Kuhakikisha shughuli zinginezo zinazotakiwa kufanywa na Baraza chini ya Sheria ya Mazingira Sura 191 zinatekelezeka.
MAWASILIANO
Unaweza kufika au kuwasaliana na Ofisi kwa anuani ifuatayo:
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) – Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jengo la NHIF, Ghorofa ya Pili
S.L.P. 6215, Mbeya, Tanzania.
Simu: 0754 779510
Barua pepe: nemcmbeya@nemc.or.tz