KANDA YA MASHARIKI KUSINI

UTANGULIZI

Kanda ya Mashariki Kusini ilianzishwa mwaka 2020 kwa ajili ya kuhudumia Manispaa ya Kigamboni, mkoa wa Dar es salaam na Wilaya za Mkuranga, Kisarawe, Kibiti na Mafia za mkoa wa Pwani. Ofisi ya Kanda ya Mashariki Kusini inapatikana katika ofisi za NEMC Makao Makuu, Kitalu namba 29/30, Reagent Estate, Mikocheni, Dar es salaam.

Uanzishwaji wa Kanda ya Mashariki Kusini ulilenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Baraza kwa ufanisi zaidi, hasa kwa kuboresha utoaji wa huduma kupitia kanda hii na kuhakikisha kuwa huduma za mazingira zinatolewa karibu zaidi na jamii. Kanda hii inachukua eneo lenye jumla ya kilomita za mraba 8,792.9 na ina jumla ya wakazi 1,271,979 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

NGUVU YA KANDA

Mazingira ya kanda yanajumuisha mchanganyiko wa mifumo mbalimbali ya ikolojia, ikiwemo mazingira ya majini (maji baridi na maji chumvi/bahari) na ya nchi kavu yenye vilima, mabonde na tambarare. Mazingira haya yanatoa fursa mbalimbali za uwekezaji katika maeneo ya viwanda na kilimo, uchakataji wa mazao ya kilimo, kilimo cha kibiashara, madini, utalii, benki, maghala ya mafuta, masoko na maduka ya kisasa, maghala ya kuhifadhia bidhaa, na maendeleo ya ardhi na majengo (real estate).

MAJUKUMU YA KANDA

Ofisi ya Kanda ya Mashariki Kusini ina jukumu la kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 (EMA, Sura ya 191) pamoja na kanuni zake katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Kanda hii inatoa huduma zifuatazo: -

·       Kusajili miradi ya uwekezaji na kusimamia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na ukaguzi wa Mazingira;

·       Kukuza uelewa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa jamii;

·      Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa mamlaka mbalimbali za serikali zilizopo katika kanda kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira na kusaidia taasisi na asasi mbali mbali zinazoshughulika na usimamizi wa maliasili na mazingira;

·       Kufanya chunguzi (surveys) zitakaosaidia usimamizi na uhifadhi wa mazingira unaofaa;

·       Kusimamia udhibiti na utekelezaji wa viwango vya ubora wa mazingira kitaifa;

·       Kuratibu tafiti mbalimbali za usimamizi wa mazingira;

·       Kushughulikia malalamiko, matukio na maoni mbalimbali ya jamii yanayohusu Mazingira; na

·       Kuchakata maombi ya ukusanyaji, hifadhi, usafirishaji na uteketezaji wa taka hatarishi; 

MAWASILIANO

NEMC-Kanda ya Mashariki Kusini

S.L.P 63154,

Dar-es-Salaam -Tanzania

Barua pepe: dg@nemc.or.tz

Simu: 255222774889