KANDA YA KATI
UTANGULIZI
Kanda ya Kati ni moja kati ya Kanda 13 za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inayosimamia Mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa ambapo ofisi zake zipo Jengo la Kambarage Tower, Mtaa wa Kikuyu, ghorofa ya Sita.
Kanda hii ilianzishwa mwezi Februari, 2018 ikiwa na jukumu la kutoa huduma katika mikoa mitatu ya Singida, Dodoma na Tabora. Hata hivyo, kutokana na kukua kwa huduma za Baraza, Kanda ya Kati ilibadilishiwa eneo la kiutendaji mwezi Julai, 2023 kwa kuhamisha Mkoa wa Tabora na kuujumisha Mkoa wa Iringa katika eneo lake. Hivyo, kwa sasa Kanda inasimamia eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 126,154.
NGUVU YA KANDA
Eneo linalosimamiwa na Ofisi ya kanda lina jumla ya wakazi 6,286,411 kwa mujibu wa sensa ya Mwaka 2022. Kiujumla eneo hili limekuwa ni kivutio cha watu wengi ambapo shughuli za kiuchumi katika nyanda za kilimo, viwanda, ufugaji, uchimbaji madini, uvunaji wa mazao ya misitu, ujenzi wa nyumba za biashara na makazi hufanyika kwa kiwango cha juu, hali ambayo imepelekea mabadiliko ya kiuchumi, kimazingira na kijamii. Aidha, katika baadhi ya maneneo kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Pori Tengefu la Mkungunero na Swagaswaga yamekuwa yakivutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mabadiliko ya kimazingira yamesababisha kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na pia mifumo ya kiekolojia kupunguza uwezo wa kutoa huduma zinazotakiwa (ecosystem services). Hali hii inahatarisha upatikanaji wa faida zitokanazo na mifumo imara ya kiikolojia na uhifadhi wa mazingira kama vile chakula, maji safi, hali nzuri ya hewa, nishati, mazao ya misitu, malisho ya wanyama pamoja na maeneo ya shughuli za kijamii na burudani.
Kwa eneo la Kanda ya Kati kilimo, ufugaji na madini zinafanyika kwa kiwango kikubwa. Aidha, shughuli za viwanda zinaendelea kukua katika maeneo ya jiji na manispaa kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu na ogezeko la watu.
MAJUKUMU YA KANDA
- Ofisi ya Kanda inamwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika kutekeleza Sheria ya Mazingira Sura 191. Majukumu mahsusi ni pamoja na:
- Kukuza uelewa kuhusu sheria ya mazingira kwa wadau;
- Kuhakikisha uzingatiaji na utekelezaji wa sheria ya mazingira;
- Kuratibu mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira;
- Upelembaji wa mazingira na mifumo ikolojia;
- Kuhakikisha changamoto za mazingira zinapatiwa ufumbuzi wa njia ya tafiti na uanzishwaji wa miradi ya kimazingira;
- Uratibu wa shughuli za mazingira kwa shughuli za kisekta na wadau mbalimbali;
- Kuhakikisha shughuli zinginezo zinazotakiwa kufanywa na Baraza chini ya Sheria ya Mazingira ya Sura Na. 191 zinatekelezeka.
MAWASILIANO
Unaweza kufika au kuwasaliana na Ofisi kwa anuani ifuatayo:
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) – Kanda ya Kati, Jengo la Kambarage, S.L.P. 2724, Dodoma, TANZANIA.
Simu: 0713 608930
Barua pepe: nemcdodoma@nemc.or.tz