WAZIRI MKUU AHIMIZA UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA- DODOMA


WAZIRI MKUU AHIMIZA UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA- DODOMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo amewaongoza wakazi wa Dodoma katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika mji wa serikali Mtumba. Katika katika hafla hiyo ya uzinduzi ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo pamoja na viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Mkoa.

Mhe. Majaliwa amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais na ikishirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Amesema "suala la kupanda miti na kuitunza ni la muhimu kwa ustawi wa Mazingira ya Taifa letu hatua inayokwenda sambamba na uhimili wa mabadiliko ya tabianchi lakini pia unawezesha mazingira ya Miji yetu kuwa ya kijani na mandhari nzuri ya kuvutia.

Sambamba na hayo Mhe. Majaliwa ameagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, timu ya wataalamu pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu kusimamia kikamilifu ujenzi wa mji wa serikali pamoja na programu ya upandaji miti pamoja na kuelimisha jamii juu ya upandaji bora wa miti kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika ili upandaji uwe na tija.