WAZIRI JAFO AWATAKA MAAFISA MAZINGIRA NCHINI KUSIMAMIA SHERIA YA MAZINGIRA KWENYE MAENEO YAO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza maafisa mazingira katika halmashauri zote kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika maeneo yao.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kikao na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Aprili 18,2024 jijini Dodoma.
“Niwatake maafisa Mazingira wote nchini wa Serikali za mitaa na kwenye taasisi mbalimbali wahakikishe kuwa wanasimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira katika maeneo yao ili kuisaidia nchi yetu katika kutunza mazingira” Amesema Waziri Jafo.
Amesema Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeanishisha wazi kuwa maafisa hao wanapaswa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa mazingira kwa Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC kwa ajili ya ufuatiliaji.
Aidha, kutokana na changamoto mbalimbali za kimazingira hususan kelele na mitetemo, Dkt. Jafo amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais katika upangaji wa miji ili kuondoa changamoto ya kelele katika maeneo ya makazi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mwongozo wa Udhibiti wa Kelele na Mitetemo ya 2021 kwa kipindi cha miaka miwili Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria NEMC Dkt. Thobias Mwesiga amesema kuwa elimu imeendelea kutolewa na malalamiko yanapokelewa na hatua zimeendelea kuchukuliwa.
“Baraza limeendelea kupokea malalamiko yanayohusu kelele chafuzi za mazingira kutoka kwa wananchi na kuchukua hatua mbalimbali kama kufanya kaguzi eneo husika kujiridhisha kwa kuchukua vipimo, kuwaita walalamikiwa kuwasikiliza na kuwapa maelekezo na kutoa adhabu stahiki kwa mujibu wa Sheria.” Amesema Dkt. Mwesiga.
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15