WACHIMBAJI WADOGO WAPATIWA ELIMU KUEPUKANA NA MADHARA YATOKANAYO NA MATUMIZI YA ZEBAKI KWENYE WIKI YA MADINI, DODOMA


Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki inayotumika kuchenjulia dhahabu ili wajiepushe na madhara yanayotokana na matumizi holela ya kemikali hiyo ikiwemo magonjwa ya ngozi, figo, saratani, kifua na hata kifo.

Hayo yameelezwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia mkuu wa serikali wakati wakitoa semina ya matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwenye Maonesho ya Wiki ya Madini Jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji wadogo (EHPMP), Dkt. Betrina Igulu amesema wachimbaji wadogo wengi hawakuwa na uelewa wa madhara ya kemikali ya Zebaki na ndiyo maana wengi wao wameathirika na matumizi ya kemikali hiyo bila kujua.

Amesema wengi wao wanatumia kemikali hiyo bila kuchukua tahadhari zozote za kiusalama kama vile kuvaa mavazi yanayowakinga kugusana na kemikali hiyo, kuvaa glove mikononi, barakoa na mabuti na hivyo kujikuta wanaathirika na kemikali hiyo baada ya kipindi cha muda mrefu.

“Serikali haijapiga marufuku matumizi ya zebaki kwenye migodi lakini inatakiwa itumike kwa tahadhari kubwa ili isilete madhara kwenye afya zenu na mazingira, kwa sababu unaweza ukadhani kuwa unatafuta fedha lakini hata ukiipata usiitumie kwa raha kwa sababu unakuwa na magonjwa yanayotokana na kemikali hiyo,” amesema Dkt. Befrina na kuongeza kuwa,

“Pia mnatakiwa kutumia zebaki kulingana na kiwango kilichoidhinishwa na shirika la afya duniani cha asilimia 15 tu kwani tulifanya utafiti kwa kushirikiana na Wizara ya afya kwa wachimbaji wadogo wa Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Mbeya na Singida ambapo tuligundua kuna matumizi makubwa ya kemikali ya zebaki hadi asilimia 60 na baadhi ya watu wameshapata magonjwa yanayotokana na kemikali hiyo.” amesema Dkt. Befrina.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kati Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bw. Gerald Mollel amewataka wachimbaji hao kuhifadhi na kutumia kwa usahihi kemikali zote zinazotumika migodini.

Aidha amesema matumizi mabaya ya kemikali hizo ni hatari kwa afya zao kwani madhara hayataonekana haraka lakini baada ya miaka 10 ndipo yatakapoanza kuonekana ikiwemo kutetemeka mikono, miguu na kichwa, ngozi kubabuka, saratani na hata kifo.

Amesema hata kama wanatafuta fedha lakini wachukue tahadhari ya kulinda afya zao ili fedha watakazozipata waweze kuzitumia kwenye malengo waliyoyakusudia badala ya kutumika kujiuguza.

Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP) ni mradi unaolenga kupunguza au kuondoa kabisa matumizi ya Zebaki nchini ili kuepukana na madhara yatokanayo na matumizi ya kemikali hiyo kwa afya ya binadamu na Mazingira.