Waziri Zungu: kufunga kiwanda siyo kipaumbele


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano maalum uliowahusisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Sekta Binafsi (TPSF) Waziri Zungu alisema kuwa kufungia kiwanda ambacho kimekiuka kanuni na sheria za mazingira inapelekea serikali kukosa mapato na hata ajira kwa vijana wa kitanzania.

“Malengo ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025, hatuwezi kufikia malengo hayo kama tutafikiria kufunga kila kiwanda ambacho kitakiuka sheria na kanuni za mazingira. Njia ya majadiliano, onyo na faini zinaweza kuleta suluhu bora zaidi bila kuathiri uzalishaji kiwandani na serikali kupata mapato,’’ alisema Waziri Zungu.

Waziri Zungu alisema kuwa Wizara yake itaendelea kukutana na wadau wa sekta binafsi ili kuendelea kutatua changamoto za kiuwekezaji na kuweka mazingira rafiki zaidi ya ufanyaji biashara hapa nchini.

“Kama wizara kupitia NEMC tutaendelea na utaratibu wa kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara ili kuangazia changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi hali ambayo itachangia katika kuleta uwazi na uwajibikaji kwa idara zetu,’’ alisema.

Aidha alisema kuwa, changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) imepatiwa ufumbuzi kwani muda siyo mrefu kuanzia sasa vibali hivyo vitapatikana kwa njia ya mtandao (Online registration).

“Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha uwekezaji unafanyika lakini pia mazingira yetu yanaendelea kuwa salama kwa faida ya kizazi cha leo na kesho. Wizara ipo katika majadiliano na idara zingine za serikali na muda siyo mrefu tutakuja na mpango wa utaoajiwa vibali kwa njia ya mtandao hali ambayo itaharakisha upatikanaji wake na kupunguza usumbufu,’’ alisema Waziri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amewataka wadau wa sekta binafsi, wawekezaji na wataalam elekezi kufanya kazi kwa ukaribu na Baraza hilo ili kuondoa kero.

“Suala la utoaji vibali ni mchakato unaoanzia kwa mwekezaji kisha mtaalam elekezi na mwisho ni NEMC. Matatizo huanza hapo kwa kuwa NEMC lazima ijiridhishe kabla kibali hakijatolewe. Nitoe wito kwa wadau wote kushirikiana na NEMC kwa hatua zote muhimu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma,’’ alisema Dkt. Gwamaka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Bw. Godfrey Simbeye amepongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa rafiki.

“Utoaji wa vibali kwa njia ya mtandao utaharakisha upatikanaji wake na kupunguza urasimu lakini pia hata ufungaji wa viwanda ambao ulikuwa ukifanyika huko nyuma ulionekana kuathiri wawekezaji, wafanyakazi pamoja na serikali, hivyo tunapongeza jitihada hizo na tunaomba majadiliano yawe ya mara kwa mara kati ya serikali na sekta binafsi,’’ alisema.

Mkutano huo maalum kati ya Waziri Zungu na wadau wa TPSF ni mwendelezo wa majadiliano kati ya NEMC na wawekezaji katika kutafuta namna nzuri ya kuondoa changamoto za uwekezaji hapa nchini.

Mwisho.