​NEMC KUFANYA MAPITIO YA ATHARI ZA MAZINGIRA KWENYE MIRADI


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limejipanga kufanya mapitio ya miradi yote ili kuangalia kama imefanyiwa Tathmini ya athari za mazingira katika kukabiliana na hatari za kimazingira zinazotokana na shughuli za miradi hiyo.

Ofisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC, Bw.Innocent Makomba akizungumza jana na waandishi wa habari kwenye maonesho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika jijini hapa, alisema lengo ni kuangalia miradi iliyofanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na ambayo haijafanyiwa tathmini hiyo ili ifanyiwe.

“Lengo ni kuhakikisha athari za mazingira haziharibu ardhi yetu, ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame, tutakachokwenda kufanya kwenye miradi yote iliyofanyiwa tathmini, ni pamoja na kuangalia masharti waliyopewa na Mheshimiwa Waziri kama yanazingatiwa,”alisema.

Alisema NEMC itaendelea kutekeleza maelekezo ya viongozi katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya mazingira ili kuhakikisha urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa unafanikiwa.

“Tutahakikisha Sheria yetu inasimamiwa kikamilifu ikiwamo kufanyika kwa Tathmini ya athari za mazingira kwa miradi yote inayokwenda kutekelezwa,”alisema.

Kuhusu vifungashio kuchangia uchafuzi wa mazingira, Ofisa Mazingira huyo alisema NEMC itaendelea kusimamia Kanuni ya mwaka 2022 iliyoweka katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

“Kwasasa tunaendelea na oparesheni kwenye viwanda maana huko ndo shina lilipo, lakini pia watanzania tubadilike tunapokwenda kufanya manunuzi tubebe mifuko yetu ili kuepuka kutumia vifungashio kama mifuko ya plasiki iliyokatazwa,”alisema.

Alitoa rai kwa viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo kuacha mara moja na NEMC haitasita kuvichukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

“Vifungashio hivi vina athari maana wakati mwingine vinafungashiwa chakula cha moto, inayohatarisha mtu kupata saratani,”alisema.

Naye, Ofisa Mazingira Mkuu kutoka NEMC, Bi.Pendo Kundya, alisema katika maonesho hayo wametoa elimu kwa umma na kupokea maoni namna ya kuboresha mazingira nchini.

“Tumetoa elimu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na NEMC kama vile tathmini ya athari kwa mazingira, tafiti zinazofanywa za mazingira, udhibiti wa kelele, mifuko ya plastiki na uzingatiaji wa sheria ya mazingira,”alisema.

Alisisitiza wananchi kupenda mazingira na kuyatunza kwa kuwa kila mwananchi ana jukumu hilo na sio kuiachia serikali peke yake