​NEMC YAWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUFANYA MATUMIZI SALAM YA KEMIKALI YA ZEBAKI ILI KULINDA AFYA NA MAZINGIRA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lawataka wachimbaji wadogo wa madini kutumia njia mbadala ya uchenjuaji na kuacha matumizi ya kemikali ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu na Mazingira.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan Jangu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na athari za matumizi ya zebaki kwa afya ya binadamu na Mazingira mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza.

Dkt. Menan amesema zaidi ya watu takribani milioni 1.5 nchini wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ambao wengi wao wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni rahisi na bei nafuu katika shughuli za uchenjuaji madini lakini ina madhara makubwa kwa kusababisha magonjwa kama kansa, utindio wa ubongo na matatizo katika mfumo wa uzazi wa binadamu.

“Zaidi ya watu takribani milioni 1.5 wanajishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ambao wengi wao wanatumia kemikali ya zebaki ambayo ni rahisi kuitumia lakini ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu kama kansa, kuharibu mfumo wa uzazi na kusababisha ugonjwa wa utindio wa ubongo, ndio maana Baraza tumejikita kutoa elimu kwa watumiaji hao kuacha kuitumia au endapo itatumiwa wavae vifaa vya kujikinga na kemikali hiyo ambayo ni hatarishi kwao na Mazingira “ amesema Dkt. Menan.

Pamoja na hayo Dkt. Menan Ameongezea kuwa Baraza kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Mfuko wa GEF wanaendelea kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya zebaki na linasisitiza shughuli zote za madini zifanyike katika utaratibu ambao hautakuwa hatarishi kwa jamii na Mazingira.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP) Mhandisi Dkt. Befrina Igulu ameongezea kwa kusema Baraza linaitaka Jamii ichukue tahadhari ya matumizi ya zebaki ambayo ni hatari na endapo itatumiwa itumike kwa utaratibu maalumu, Pia ametoa wito kwa wamiliki mialo kuwa na vifaa kinga kwa wachenjuaji ili waweze kujikinga na kemikali ya zebaki hii itasaidia kupunguza athari kwa mifumo ya ikolojia, afya ya jamii na Mazingira.