NEMC YATOA SOMO KWA NCHI 34 NAMNA YA KUTEKELEZA MIRADI YA MABADILIKO YA TABIANCHI
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepongezwa kwenye mkutano wa kimataifa uliozikutanisha Nchi 34, wa kujengeana uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa matumizi mazuri ya fedha za miradi ya kuhimili mabadiliko hayo.
Akizungumza jana kuhusu mkutano huo, Mratibu wa Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) Tanzania, Fredrick Mulinda, alisema Nchi hizo pamoja na sekretarieti ya mfuko huo, zimepongeza na kujifunza mbinu ambazo NEMC imezitumia katika utekelezaji wa miradi na kuahidi kutumia ujuzi huo kwenye mataifa yao.
Alisema NEMC imepewa dhamana ya kusimamia fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania kutoka kwenye mfuko huo na ilipewa uenyeji wa mkutano huo.
“Mkutano huu ulihusisha taasisi kutoka nchi 34 ambazo zina majukumu kama ya NEMC, tumekutana Dodoma na huu ni utaratibu uliowekwa na sekretarieti ya mfuko kila mwaka kukutanisha taasisi hizo ili kushirikishana uzoefu na ujuzi kwenye utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi,”alisema.
Alisema NEMC iliwasilisha taarifa ya miradi miwili inayotekelezwa wilaya ya Kongwa, Bahi, Manyoni na Nzega na imejikita katika kukabiliana na ukame kwa wakulima na wafugaji.
“Wageni wametembelea Kongwa mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima na wafugaji, Mradi wa uvunaji maji kimkakati kuhimili mabadiliko ya tabianchi Bahi na baada ya hapo tulienda Arusha kwenye mkutano wa kuruhusu taasisi zingine za mataifa mbalimbali kueleza yanayofanyika kwenye nchi zao,”alisema.
Alisema mkutano huo umewezesha NEMC kuonesha Tanzania inavyokabiliana na mabadiliko hayo na umefungua fursa za utalii sambamba na kuijengea Tanzania imani kwa mfuko huo kutokana na matokeo makubwa yaliyoonekana katika miradi.
“Pia Tanzania ilipata fursa ya kufikisha ajenda ya kuharakisha mchakato wa kuidhinisha ithibati ya pili kwa NEMC kwa Adaptation Fund. NEMC imepewa dhamana ya kusimamia fedha hizi lakini kila baada ya miaka mitano huwa yanafanyika mapitio na yanapokamilika ndio hutolewa ithibati, sasa NEMC inasubiri ipate ithibati ya pili ili iombe fedha zaidi, sekretarieti imeahidi kushughulikia kwa haraka,”alisema.
Akitoa neno la ukaribisho kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, alisema Baraza litajifunza na kubadilishana ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko hayo ili kuendeleza jitihada hizo nchini.
“Warsha hii itakwenda kuwa chachu kwa taifa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,”alisema
-
Maazimisho
2020-01-21
-
Kongamano la Kisayansi
2023-08-28
-
Wiki ya Utumishi wa Umma
2019-12-15