​NEMC, GCLA YAENDESHA MAFUNZO YA USIMAMIZI NA UDHIBITI WA KEMIKALI KWA WACHIMBAJI WADOGO MAMLAKA YA MJI MDOGO MAKONGOLOSI WILAYANI CHUNYA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Tume ya Madini Mkoa wa Mbeya wameendesha mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo waliopo katika Kata za Makongolosi, Bwawani na Mkola zilizopo katika Mamlaka ya mji mdogo Makongorosi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Mafunzo hayo yameendeshwa kupitia Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo (EHPMP) unaoratibiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mhandisi Boniface Kyaruzi kutoka NEMC amesema wanaendesha mafunzo hayo kukumbushana wajibu uliopo kwa wachimbaji wadogo kwenye suala zima la usimamizi wa matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji hao

Amesema Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha madhara ya matumizi ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji yanadhibitiwa kwa kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Minamata pamoja na kuwepo kwa Sheria zinazotoa miongozo ya utekelezaji wa matakwa ya mkataba huo ikiwemo Sheria ya Mazingira, Sheria ya Kemikali iliyopo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Kanuni mahususi za zebaki kwa ajili ya kutekeleza mkataba huo