​ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA ZEBAKI YAWAFIKIA WACHIMBAJI WADOGO TAKRIBANI 600 MKOA WA MARA


Elimu ya matumizi salama ya zebaki kwa wachimbaji wadogo inayotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Madini yawafikia wachimbaji wadogo takribani 600 Mkoa wa Mara

Elimu hiyo inayotolewa kupitia Mradi wa kudhibiti matumizi ya Kemikali ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wanaotumia kemikali ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu unaofadhiliwa na Bank ya Dunia imelenga kuainisha sifa za zebaki, namna inavyoingia mwilini, madhara yatokanayo na matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu ,namna ya kujikinga na athari pamoja na namna ya kuihifadhi.

Akitoa elimu hiyo kwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Mara iliyohusisha wachimbaji kutoka machimbo ya Nyangoto, Kenyamanyori na Irasamilo Meneja kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw.Musa Kuzumila amesema elimu hii ni katika kutekeleza Mkataba wa Minamata wenye takwa la kuwa na mpangokazi wa utoaji elimu ya matumizi salama ya zebaki kwa wachimbaji wadogo.

Amesema Zebaki madhahara yake ni kuharibu mfumo wa fahamu unaopelekea ulemavu wa viungo, Figo, kuhisi, msongo wa mawazo, ngozi kuharibika, mimba kwa wanawake kuharibika, kuzaa watoto wenye ulemavu na kupoteza nguvu za kiume.

Bwana Kuzumila pia amezitaja njia za kuzuia madhara wakati wa uchenjuaji kuwa ni kutumia vifaa kinga kama gloves, barakoa, respirator, overall, mabuti, miwani na helmet wakati wa uchenjuaji.

Ameongeza kuwa zebaki inatakiwa kuhifadhiwa vizuri kwa kuzingatia lebo kusomeka kwa lugha ya kiswahili na kingereza, isihifadhiwe nyumbani, isiwekwe karibu na tindikali, Ammonia au Metal, iwekwe kwenye kifungashio, ufuniko wa chupa ufungwe vizuri na itunzwe kwenye eneo kavu na lenye mzunguko mzuri