​ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA ZEBAKI YATUA KIJIJI CHA RWAMGASA-GEITA


Elimu ya matumizi salama ya zebaki imetolewa kwa wachimbaji wadogo walioko Kata ya Rwamgasa Kijiji Cha Lwamgasa Wilaya ya Geita vijijini Mkoa wa Geita.

Akitoa elimu hiyo yenye lengo la kujenga utambuzi wa madhara ya matumizi ya kemikali ya zebaki na namna ya kujikinga Bw.Musa Kuzumila, Meneja wa usajili wa kemikali na Maabara za Kemia kutoka ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema elimu hii ni katika kutekeleza mkataba wa Minamata wenye takwa la kuandaa mpango kazi wa namna sahihi ya kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo.

Ameongeza kuwa matumizi yasiyo salama ya kemikali ya zebaki huleta athari za kiafya ambazo ni kuharibiwa kwa mfumo wa fahamu na viungo muhimu vya mwili hali inayopelekea kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho kuharibika, kushindwa kufanya kazi, kupoteza nguvu za kiume, msongo wa mawazo, kuwashwa kwa ngozi na mwili kudhoofika,

Naye Bw. Dereki Masako, Mkemia kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alipozungumza amesema zebaki iko katika hali ya kimiminika kizito na ni moja kati ya vyanzo kumi vinavyohatarisha zaidi afya ya jamii kutokana na shughuli za kibinadamu

Ameongeza kuwa inauwezo wa kusafiri masafa marefu, hudumu kwa miaka mingi, hujilimbikiza katika mfumo mfuatano wa chakula na huleta madhara kwa afya na mazingira.

Bw.Dereki amesema kemikali ya zebaki huingia mwilini kwa njia ya hewa, kupitia ngozi au macho, kula au kumeza na kupitia tumbo la uzazi la Mama na kuwataka wachimbaji kutumia vifaa Kinga kama gloves, miwani, mabuti, koti, kofia, reflector, barakoa au respirator na kizimamoto ili kujikinga na athari za kiafya zinazoweza kutokea.

Naye Bwa.Zakaria Deus, Afisa Mteknolojia kutoka Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya ziwa alipozungumza ameeleza usimamizi na uhifadhi wa zebaki kuwa uzingatie kusomeka kwa lebo ikiwa na lugha ya kiswahili na kiingereza, ihifadhiwe vizuri, isitunzwe nyumbani, ifunikwe kwenye vifungashio, itunzwe kwenye eneo kavu na lenye mzunguko mzuri na isitunzwe karibu na tindikali, Ammonia na Metal

Katika hatua nyingine Bi Hyasinta Laurean kutoka Tume ya Madini-Geita alipohojiwa alikiri kufurahishwa na elimu ya matumizi salama ya zebaki inayoendelea na kuwataka wachimbaji wa Rwamgasa kuzingatia hilo ili kulinda afya yao na afya ya Mazingira