Waziri Zungu apongeza kiwanda kwa kurejeleza chupa za plastiki na kuuza nje


Akizungumza kiwandani katika eneo la Mbagala jijini hivi karibuni, Waziri Zungu ameupongeza uongozi wa Kampuni ya A-One Products & Bottlers Ltd kwa uwekezaji wa kurejeleza chupa za plastiki ambazo amesema tayari zimekuwa tatizo la kitaifa la uchafuzi wa mazingira.

Ametoa pongezi hizo baada ya kupokea mealezo ya Afisa Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bwana C. B. Reddy juu ya jitihada ya kampuni ya kubadilisha taka ngumu kuwa mali yenye manufaa kwa taifa.

Bw Reddy ameihakikishia Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba kiwanda kina utaalaamu na vifaa vya kisasa vya kurejeleza chupa plastiki za bluu na nyeusi zilizotumika na kuibua malighafi ambayo ina soko zuri Namibia, Afrika ya Kusini na Nchi za Falme za Kiarabu. “Tuna soko huko Italia. Ilikuwa tupeleke mali kwa wateja wetu huko lakini haikuwezekana kwa sababu ya kuibuka kwa uogonjwa wa Corona,” ameeleza Bw Reddy.

Amesema kampuni yake imezalisha ajira isiyokuwa ya moja kwa moja kwa Watanzania wanaojituma na kukusanya chupa za plastiki zilizotumika hasa katika Jiji la Dar es Salaam na kutaja vituo vinavyopokea chupa hizo kuwa ni Mbezi Jogoo katika Wilaya ya Ubungo na Shekilango katika Wilaya ya Kinondoni.

Waziri Zungu amewataka Watanzania wachangamkie fursa za aina hii zinazojitokeza na kusema kwamba fursa hizo ni matokeo ya juhudi ya serikali ya awamu ya tano ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara. “Watanzania wenzangu tumieni fursa hizi kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa,” amesema waziri, na kuongeza kwamba iwapo vijana watachangamkia fursa hii watajiajiri na kupunguza sana chupa za plastiki zinazochafua mazingira.

Bw Zungu ameiambia hafla hiyo kwamba ujumbe wake umefanya ziara ya siku moja kujionea wenyewe jitihada ya kurejeleza chupa za plastiki zilizotumika. “Kuna maneno yanayosikika mitaani kwamba chupa za juisi zenye rangi ya bluu na nyeusi zinazagaa mitaani kwa kuwa haziwezi kurejelezwa. Sisi kama Baraza lenye dhamana ya mazingira tukaamua tuje kwenye kiwanda hiki tujiridhishe, iwapo kiwanda hiki hakipokei chupa hizo.”

Waziri Zungu amesema serikalil itashirikiana na wenye viwanda vyenyekurejeleza taka ngumu kuhakikisha Sheria mama ya Mazingira ya mwaka 2004, na hasa Kanuni za udhibiti wa taka ngumu za Mwaka 2009 zinazingatiwa ili mazingira yawe salama.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, amewaomba wananchi wakusanye chupa za plastiki zilizotumika, waziuze na kujikwamua kiuchumi kwani kilo moja inanunuli shilingi 400. Amesedma mjasiriamali atakayekusana tani moja na kuendelea atapewa fedha ya usafirishaji kiasi cha 35,000/- baada ya kufikisha mzigo kiwandani.

“Wajasiriamali na wadau wa mazingira wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa kama hizi. Fursa ina kipato kizuri pia ni njia moja wapo ya kutunza mazingira kwa maisha ya sasa na vizazi vya baadae,” amesema Dk. Gwamaka.

Katika ujumbe huu, alikuwemo mwanaharakati wa mazingira, Bi Neema Clarence na Katibu wa Mwenezi wa CCM, Wilaya ya Ilala, Bw Sultani Saidi.

Mwisho/