​WANANCHI WASISITIZWA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NA KUACHANA NA NISHATI CHAFUZI


Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo yote nchini wamesisitizwa matumizi ya Nishati safi ya kupikia na kuacha matumizi ya nishati chafuzi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bi. Christina Mndeme alipokuwa akizindua Kongamano la β€œπ‘Ίπ‘¨π‘΄π‘°π‘¨ 𝑡𝑰𝑺𝑯𝑨𝑻𝑰 𝑺𝑨𝑭𝑰 𝑭𝑬𝑺𝑻𝑰𝑽𝑨𝑳” lenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki kwa Mazingira na afya ya viumbe hai.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kongamano hilo Bi. Christina Mndeme amesema nishati safi kama matumizi ya umeme, gesi na joto la ardhi ni nyenzo kuu kwa Taifa letu kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi pia amewaasa Wananchi kuacha matumizi ya nishati chafuzi kama mkaa na kuni ambazo zinaharibu mazingira, kusababisha magonjwa ya upumuaji, vifo na athari nyingine za kijamii.

β€œNaomba niseme kuwa Nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, nishati chafuzi kama kuni na mkaa zinasababisha uharibifu wa Mazingira, vifo kwa watoto wachanga, magonjwa ya upumuaji na changamoto katika familia kama ndoa kuvunjika, hivyo ndugu zangu natoa wito kwa Viongozi wote wa Chama na wananchi wote suala la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ni jukumu la kila mtu” amesema Bi. Christina Mndeme.

Naye Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira NEMC Dkt. Menan Jangu Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC amesema Baraza lipo tayari kushirikiana na vikundi, wadau na Taasisi mbalimbali kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na kuhakikisha matumizi ya kuni na mkaa yanapungua kufikia mwaka 2034.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki ufunguzi wa Kongamano hilo, washiriki wengine ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Janeth Maurice Massaburi, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), STAMICO na SESCOM.