TUJENGE UTAMADUNI WA KUTUNZA MAZINGIRA KWA KUPANDA MITI -Dkt. JAFO.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selaman Jafo amewataka wananchi waishio eneo la hifadhi ya msitu wa Pugu Kazimzumbwi na Watanzania kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kulinda Mazingra yao kwa kupanda miti.

Waziri Jafo amebainisha hayo mara baada ya kutembelea hifadhi hiyo iliyopo Wilayani Kisarawe nakujionea vivutuo mbalimbali vya utalii ndani ya hifadhi hiyo.

"Kuongezeka kwa joto Ulimwenguni umechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mabadiliko makubwa kwenye mazingira hivyo ni jukumu la watanzania wote kuwa na ajenda moja ya kupanda miti ili kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. "Amesema Dkt.Jafo

Aidha Waziri Jafo amesema kutunzwa kwa hifadhi ya msitu wa Pugu Kazimzumbwi itasaidia kuongeza chachu kwenye Sekta ya Utalii nakufanya mji wa Kisarawe kujulika ndani na nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka amesema ni jukumu la kila mwananchi kuona umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa Upande wake Kamanda Msaidizi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki Caroline Malundo amesema kutunzwa kwa hifadhi hiyo imesaidia kuongezeka kwa watalii wanaotembelea eneo hilo kutoka watalii mia tatu(300) mwaka 2017 hadi kufikia watalii elfu kumi (10,000) mwaka 2021.

Katika ziara hiyo Waziri Jafo pia ameongoza zoezi la upandaji wa miti katika eneo la hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.