RAS IRINGA AITAKA NEMC KUUTAZAMA MTO RUAHA KWA JICHO LA KIPEKEE.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Mhandisi Leonard Masanja amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza nguvu katika kuulinda Mto Ruaha.

Mhandisi Masanja ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na watumishi wa NEMC - Kanda ya Kati walipofika Ofisini kwake ambapo kwa sasa Mkoa huo unahudumiwa na NEMC Kanda ya kati badala ya Kanda ya Nyanda za juu kusini kama ilivyokuwa awali.

“Uhifadhi wa vyanzo vya maji ukiwemo Mto Ruaha unaopita katika Mbuga ya wanyama ni eneo ambalo linatakiwa liangaliwe kwa jicho la kipekee sana” Amesema Mhandisi Masanja.

Akizungumzia kuhusiana na uharibifu unaoendelea wa vyanzo vya maji amesema Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ipo na inabidi kusimamiwa.

“Tuna vyanzo mbalimbali vya maji katika Mkoa wetu wa Iringa lakini kutokana na ukame unaojitokeza watu huvamia maeneo ya vyanzo hivyo vya maji, kuna sheria inayoelekeza shughuli zote zifanyike umbali wa mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji, hivyo ni vizuri kuisimamia” Ameongezea Mhandisi Masanja.

Naye Afisa Mazingira wa Mkoa wa Iringa Dkt. Golyama Bahat amesema kwa mwaka 2023 Mkoa wa Iringa umefanya vizuri katika upandaji miti ambapo jumla ya miti milioni 35 imepandwa hadi kufikia mwezi Julai 2023.

“Kwa mwaka huu 2023 Iringa tumepanda miti milioni thelathini na nane, ni tofauti na mwaka jana na juzi ambapo tulikuwa tunaishia kupanda miti milioni thelathini na tano kwahiyo suala la kupanda miti ni utamaduni wetu hapa Iringa.” Ameeleza Dkt. Golyama.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Careen Kahangwa ametumia fursa hii kuwakumbusha watanzania kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwani ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anatunza mazingira ili kulinda afya yake na ya jamii inayomzunguka.

Pia Dkt. Careen amewakumbusha wadau wa Mazingira wanaotakiwa kulipa ada ya Mazingira kila mwaka kuhakikisha wanafanya hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya Mazingira ya Ada na Tozo ya Mwaka 2021 inayotokana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.

Wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wapo Mkoani Iringa kuanzia Julai 17 hadi 21, 2023 kutembelea wadau wa Mazingira pamoja na kutoa elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na kukumbushia malipo ya Ada kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.