NEMC YATOA ELIMU YA UDHIBITI WA KELELE NA MITETEMO KWENYE KONGAMANO LA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE LILILOFANYIKA DAR ES SALAAM


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa elimu ya udhibiti wa Kelele na Mitetemo iliyozidi viwango kwa Maaskofu na Wachungaji wa Makanisa ya Kipentekoste ili kukuza uelewa wa Sheria ya Mazingira na Kanuni za Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015. Lengo likiwa ni kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na sauti zilizozidi viwango kwenye nyumba za ibada.

Akiongea na Viongozi hao Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Bi. Glory Kombe ametoa elimu hiyo katika Mkutano uliofanyika tarehe 8/8/2024 katika Kanisa la Naioth Makuburi lililopo Ubungo, Dar es salaam.

Bi. Glory Kombe amesema Kelele na Mitetemo iliyozidi viwango inaweza kusababisha athari kama Kupunguza umakini, kudumaza ukuaji wa watoto, matatizo ya akili, athari kwenye mimea na wanyama wote. Pia ameongeza kwa kusema kuwa ni wajibu wa viongozi wa dini zote kuendesha shughuli za ibada kwa kuzingatia Sheria ya Udhibiti kelele na mitetemo ya Mwaka 2015 ili kuhifadhi Mazingira.

“Pamoja na Kanuni husika kuweka kiwango cha sauti pale inapozidi 75dBA hiyo inakuwa ni uchafuzi ambao unaweza kupelekea athari mbalimbali kama maumivu kwenye masikio, kupunguza umakini, matatizo ya afya ya akili, athari kwenye mimea na wanyama wote. Hivyo ni wajibu wa Taasisi za kidini na nyumba za ibada kuendesha shughuli hizo kwa kuzingatia Sheria za Udhibiti wa kelele na mitetemo ili kuhifadhi Mazingira” amesema Bi. Glory Kombe

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Sheikh. Yasin Masenga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani kwa kuheshimu imani, ibada na mipaka ya dini nyingine, pia amewataka waumini hao kufuata Sheria ya Uhuru wa kuabudu iliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uongozi na waumini wa kanisa la PNI umewashukuru NEMC na JMAT kuendelea kutoa elimu ya udhibiti wa kelele na mitetemo.

Mkutano umeandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste. NEMC na JMAT wameshirikiana kutoa elimu ya Udhibiti wa kelele na mitetemo kwenye nyumba za ibada.