MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA JUU YA TATHMINI YA HALI YA MAZINGIRA YA BAHARI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango amefungua mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya hali ya mazingira ya Bahari ikiwemo masuala ya kiuchumi na kijamii ambao unajumuisha washiriki kutoka katika mataifa mbalimbali duniani,ambapo Tanzania kwa mara ya pili imekuwa mwenyeji wa mkutano huu katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Dar es salaam.

Mhe. Mpango ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika utunzaji wa bahari kwa kuzuia utumiaji wa mifuko ya plastiki, kudhibiti uvuvi wa kutumia mabomu kwa takribani asilimia 99 na kuongeza ulinzi na uangalizi katika shughuli za uvuvi. Pamoja na hayo ametoa wito wakulinda bahari ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kudhibiti taka za plastiki na uchafuzi wa bahari.

Pia amesisitiza kuwa inahitajika nguvu ya pamoja kutoka katika mataifa mbalimbali ili kuongeza juhudi katika utunzaji wa Bahari. "Ni muda sasa kutafuta njia sahihi za kusimamia na kudhibiti shughuli zinafanywa katika Bahari na jinsi ya kuleta usawa wa uhai wa bahari na ikolojia kwa maendeleo endelevu" amesema.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema" Mkutano huu utasaidia kukuza uwezo kwa watafiti wa masuala ya mazingira jinsi ya kuratibu shughuli za uchumi wa bahari na pia Tanzania kuhakikisha kuwa jamii zetu zinatumia fursa ya Bahari katika kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa bluu na UvuviSerikali ya Mapinduzi ZanzibarDkt. Aboud D. Jumbe amesema programu za umoja wa mataifa za uuvi na uhifadhi wa bahari zinaweza pamoja na taarifa sahihi za utunzaji wa mazingira ya bahari pamoja na kuchagia katika ukuaji wa fursa za kiuchumi ili kufikia maendeleo endelevu ya Bahari.

Kwa upande wake mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kitengo cha mambo ya Bahari na Sheria ya Kimataifa Bi. Alice Hicuburundi amesema uelewa ni jambo muhimu zaidi katika kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Bahari.

Kongamano hili ni muhimu katika kuwajengea uwezo Nchi washiriki katika kusimamia na kuhifadhi Bahari kwa maendeleo endelevu.