KAMATI YA KITAIFA YA USHAURI WA TAFITI ZA MAZINGIRA ITASAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA KIMAZINGIRA NCHINI: DKT. GWAMAKA


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amezungumza haya katika uzinduzi wa kamati ya kitaifa ya ushauri wa tafiti za mazingira uliofanyika mjini Morogoro, leo hii.

Dkt. Gwamaka amesema kuwa kupitia kamati hiyo tafiti mbalimbali zitafanyika kwa ajili ya kutatua changamoto za kimazingira zinazozikumba jamii zetu.

"Zipo changamoto za kimazingira katika maeneo mbalimbali, pasipo kuwa na chombo kama hiki ambacho kinaelekeza ni wapi tuweke kipaumbele lazima tutaathirika kitaifa. Kwahiyo kamati hii ipo kwa ajili ya kuratibu tafiti zote zinazohusu Mazingira kwa kusimamiwa na NEMC" amesema Dkt. Gwamaka

Kuhusu utendaji kazi wa kamati hiyo Dkt. Gwamaka amesema kuwa kamati itahitaji vyanzo vya mapato ili kuendesha shughili mbalimbali za kitafiti.

"Kamati hii tuliyounda inahitaji pia kuweza kutafuta vyanzo vya pesa kwa ajili ya kugharamia na kuziendeleza tafiti hizo. Yapo maeneo ambayo ni nyeti nchini yenye changamoto za kimazingira na yamepewa kipaumbele kufanyiwa tafiti na majibu ya tafiti tutakazofanya yatakwenda kutatua changamoto hizo" amesema Dkt. Gwamaka

Mwenyekiti aliyechaguliwa na wajumbe wa kamati hiyo Dkt. Thomas Bwana kutokaOfisi ya Makamu wa Rais amesema kuwa usimamizi na ushiriki wake katika kamati hiyo utaendeleza upatikanaji na utekelezaji wa tafiti na taarifa.

" Zipo changamoto nyingi za kimazingira ambazo zinahitaji taarifa za kiutafiti. Jukumu letu sisi ni kuhakikisha tafiti sahihi na zinazohitajika zinafanyika" amesema Dkt. Bwana

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe katika kamati hiyo Dkt. Catherine Masao, Mhadhiri Mazingira na Mshauri katika masuala ya Uhifadhi Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema atatumia nafasi yake kutoa ushauri juu ya masuala yote ya kimazingira.

"Nitaweza kushauri vizuri katika masuala ya Mazingira, mabadiliko ya tabia ya nchi" amesema Dkt. Catherine.

Kamati ya kitaifa ya ushauri wa tafiti za Mazingira imeanzishwa kwa mujibu wa Agenda ya Taifa ya Tafiti za Mazingira ya 2017-2022 ikiwa na jukumu la kuratibu Tafiti za Mazingira.

NEMC ndio wenye wajibu wa kuunda kamati hii inayohusisha wajumbe kutoka Taasisi za elimu na utafiti pamoja na taasisi nyinginge husika za Kiserikali na zisizo za Kiserikali.

Tafiti zenye viwango vya juu na mlengo sahihi ni muhimu katika kutoa taarifa sahihi kwa wafanya maamuzi na watengeneza Sera ili kuwa na mipango sahihi ya kimazingira inatayochangia maendeleo endelevu.

Mkutano huu ulishirkisha wadau mbalimbali kama Ofisi ya Makamu wa Rais, TAMISEMI, Mamlaka ya Mazingira Zanzibar, COSTECH,Umoja wa Taasisi zisizo za Kiserikali (TANGO),Vyuo vikuu vya UDOM SUA, UDSM na Chuo Kikuu cha Zanzibar.