DKT. GWAMAKA AIKUMBUSHA JAMII KUHESHIMU SHERIA YA VIWANGO VYA KELELE NA MITETEMO


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ameitaka jamii kuheshimu kanuni za viwango vya kelele na mitetemo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuepusha changamoto za kimazingira kwa wakazi wa maeneo husika.

Dkt. Gwamaka ameyasema hayo katika mkutano na wanahabari hii leo ambapo amesema kuwa kanuni ya Mazingira ya mwaka 2015 inatoa maelekezo na makatazo juu ya viwango vya sauti lakini bado watu wengi wamekuwa wakikiuka.

“Kumekuwa na wimbi la mamalamiko mengi sana ambayo yamefika kwetu.Sisi kama baraza tumekuwa tukichukua hatua na mpaka sasa hivi kuna baa kumi pamoja na nyumba za starehe tumekwisha wapiga faini na tumewapa onyo kali ambalo ni pamoja na kuwafungulia mashtaka pale ambapo watashindwa kufuata hayo masharti” amesema Dkt Gwamaka.

Dkt. Gwamaka amesisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na mitetemo, umekuwa ukifanyika bila kujali sheria za nchi na sasa NEMC inaendelea kishugulikia suala hilo ipasavyo.

Tumeona ni vizuri tukumbushe jamii kwamba kuna Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ambayo inakataza uchafuzi wowote wa kelele na mitetemo hasa kwenye maeneo mbalimbali.”amesema huku akisisitiza kuwa vipo viwango maalumu ambavyo vimewekwa na vinatakiwa kuzingatiwa. Dkt. Gwamaka ameongeza kuwa ananatoa rai kwa jamii kufuata viwango hivyo. Kuna athari nyingi sana zinatokea katika hayo maeneo.” amesema Dkt. Gwamaka.

Mkurugenzi mkuu pia amesema kuwa mtu yeyote atakaendelea kwenda kinyume cha kanuni na sheria, atachukuliwa hatua kali za kisheria ambapo kanuni hizo zimeweka vigezo na tozo maalumu kuanzia Sh milioni tano hadi Sh milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo.

Aidha Dkt. Gwamaka asema mambo mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni itakayovunjwa na kusisitiza kuwa hatua hizo zitachukuliwa ipasavyo hivyo jamii haina budi kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa katika kuyalinda mazingira yetu.