WAZIRI UMMY AZITAKA HALMASHAURI NCHINI KUSIMAMIA SHERIA YA MAZINGIRA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa kuna haja ya kuangalia mfumo mzuri wa kusimamia ajenda ya Mazingira katika ngazi ya mamlaka ya Serikali za mitaa.

Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. Ameeleza kuwa ni lazima Wilaya zote Nchini kuwa na Idara ya mazingira inayojitegemea yenye wataalam mbalimbali kwenye maswala ya mazingira.

“Nimemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais kukaa na Katibu Mkuu wa TAMISEMI na Katibu Mkuu wa Utumishi ili tuweke vizuri mfumo katika ngazi ya Halmashauri ili Idara ya mazingira iwe Idara inayojitegemea yenye wataalam mbalimbali kwenye maswala ya mazingira, lakini pia itengewe bajeti ya kutosha ili waweze kufanya shughuli za uhifadhi na utunzaji wa Mazingira” Mhe. Ummy Mwalimu.

Aidha katika ziara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amekagua machimbo ya mchanga Kata ya Kilomo, pia alitembelea mikoko katika vijiji vya Kondo na Mlingotini Wilaya ya Bagamoyo ili kujionea hali halisi ya mazingira. Akiwa katika machimbo ya mchanga ameeleza kuwa kuna haja ya kupata mchanga kwa ajili ya ujenzi lakini changamoto iliyopo kwa sasa ni baadhi ya wachimbaji wengi kuacha maeneo hayo bila kuyarejeleza yawe katika hali yake ya asili na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

“Tunatambua kuwa ipo haja ya mchanga lakini kama Ofisi ya Makamu wa Rais changamoto ambayo tumeibaini baada ya kuchimba mchanga hakuna anaefanya shughuli ya kuirejesha ardhi katika hali yake ya asili. Rai yangu kwa Halmashauri na Wilaya ni kuhakikisha tunaendelea kuwasimamia wanaochimba mchanga mara tu watakapomaliza shughuli ya kuchimba mchanga kuhakikisha wanafanya kazi ya kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwemo kusawazisha eneo hilo” Mhe. Ummy Mwalimu

Ameendelea kueleza kuwa Halmashauri za Ukanda wa Pwani wahakikishe wanalinda misitu ya mikoko kwa kushirikiana na wakala wa Misitu (TFS), lakini pia kuhakikisha wanapanda mikoko mipya ili kulinda mazingira ya Bahari na kuziwezesha jamii za Ukanda wa Pwani kuwa na shughuli nyingine za kujiingizia kipato kwani wengi wanakata mikoko ili kujipatia fedha za kujikimu

“Tunao wajibu wa kuzijengea uwezo jamii ambazo zinakaa katika Ukanda wa Pwani waweze kufanya shughuli nyingine zitakazo waingizia kipato kinyume na kukata mikoko inayotumika kwa ajili ya kujengea na kujipatia mkaa. Hivyo tunahitaji kutunza na kuhifadhi mikoko kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho”Mhe. Ummy Mwalimu alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainabu Kawawa amesema kuwa Halmashauri ya Bagamoyo inategemea sana Bahari katika shughuli za kujipatia kipato hivyo jamii itambue kuwa kunahaja ya kulinda na kuifadhi mikoko kwa manufaa ya jamii nzima

“Natoa rai kwa watu wanaoharibu mikoko kuacha mara moja kukata mikoko kwasababu wanaua mazalia ya samaki na kupelekea uchumi kwa jamii kuyumba kwani wananchi wa Bagamoyo wanategemea Bahari kama njia ya kujipatia kipato.Hivyo wale wote watakao kaidiSerikali tutawachukulia hatua kali za sheria ya mazingira inavyosema” Mhe. Zainabu Kawawa.

Waziri Ummy yupo katika ziara ya siku 3 katika Mkoa wa Pwani kuangalia hali halisi ya changamoto za mazingira katika Mkoa huo.