WAZIRI JAFO ASHIRIKI KAMPENI YA USAFI WA FUKWE ZA RAINBOW MKOANI DAR ES SALAAM


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Dkt Selemani Jafo ameshiriki kampeni ya usafi katika fukwe za Rainbow zilizopo katika Manispaa ya Kinondoni katika Mkoa wa Dar es Salaam kampeni hiyo inaitwa zero plastic ikiwa ni juhudi za kutokomeza kabisa matumizi ya plastiki.

Akiongea katika tukio hilo Mhe. Jafo amesema kuwa suala la usafi katika fukwe ni la muhimu sana kwani ni sehemu ambayo watu huenda kwa ajili ya kujipumzisha hivyo ni lazima sehemu hizo ziwe safi muda wote.

“Fukwe ni sehemu ya Wananchi kupumzika mtu ukiwa na msongo wa mawazo ukija fukweni ukiangalia maji moyo unapata Amani hivyo basi ni lazima tuhakikishe tunazitunza fukwe zetu kwa kuhakikisha mazingira yote ya mahali hapa yanakua safi na salama”

Vilevile Waziri Dkt Jafo alisisitiza kwa Taasisi zote za Serikali kutilia mkazo matumizi ya nishati mbadala na kuacha kutumia mkaa au kuni. Na kuweza kutumia nishati mbadala ili kuweza kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Niziagize Taasisi zote za Serikali kama vile Majeshi ikiwemo Magereza,Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Vyuo vyote pamoja na Shule zote za Sekondari na Msingi (Binafsi na Serikali) kuanza kutumia nishati mbadala na majiko banifu. Nimewaomba STAMICO ambao wameanza kutengeneza mkaa badala wa kutumia makaa ya mawekuongeza uzalishaji zaidi ili kuweza kutimiza mahitaji ya Wananchi wengi.”

Aidha kwa upande mwingine pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Dkt Selemani Jafo amezindua kampeni hiyo ya zero plastic kwa kuhamasisha Wananchi kutumia vifaa mbalimbali vinavyotengenezwa kwa kutumia miti ya mianzi kama vile miswaki, vikombe na mirija ya kunywea vinywaji mbalimbali. Vifaa hivyo vilikua vikionyeshwa katika uzinduzi huo ambapo Wananchi wamepata fursa yakuviona na kujifunza.

Naye Balozi wa Mazingira aliyeandaa kampeni hiyo ya zero plastic Laura Kivuyo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Vijana katika suala zima la utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira na kuhamasisha Jamii kuendelea kutunza na kuhifadhi Mazingira.